Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wakimbizi milioni 7 duniani kote hawako shuleni- UNHCR

Mwanafunzi kutoka Sudan Kusini akiwa darasani katika shule moja nchini Kenya.
© UNHCR/Charity Nzomo
Mwanafunzi kutoka Sudan Kusini akiwa darasani katika shule moja nchini Kenya.

Watoto wakimbizi milioni 7 duniani kote hawako shuleni- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya nusu ya watoto milioni 14.8 wakimbizi duniani kote wenye umri wa kwenda shuleni, hawako shuleni na hivyo kuhatarisha mustakabili wao wa ustawi na kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR.

Ripoti hiyo ya elimu kwa wakimbizi mwaka 2023 imetolewa leo Geneva, Uswisi na inakusanya takwimu kutoka zaidi ya nchi 70 zinazohifadhi wakimbizi. 

Mathalani inabainisha kuwa mwishoni mwa mwaka 2022, idadi ya wakimbizi watoto wenye umri wa kwenda shule iliongezeka kwa asilimia 50 kutoka watoto milioni 10 mwaka uliotangulia, ikichochewa na vita nchini Ukraine. 

Asilimia 51, sawa na zaidi ya watoto milioni 7 hawajaandikishwa shuleni. 

Wanawake vijana waliokimbia Afghanistan wahudhuria mafunzo Pakistan.
© UNHCR/Mercury Transformations
Wanawake vijana waliokimbia Afghanistan wahudhuria mafunzo Pakistan.

Ukipanda juu fursa zinapungua zaidi 

Ripoti hiyo inasema uandikishwaji wa watoto shuleni unatofautiana kulingana na kiwango cha darasa katika kila nchi, ambapo asilimia 38 wameandikishwa elimu ya chekechea, asilimia 65, elimu ya msingi, asilimia 41 elimu ya sekondari na ni asilimia 6 peke elimu ya juu. 

“Katika nchi za kipato cha chini, tofauti ya viwango vya uandikishwaji shuleni miongoni mwa wakimbizi na wasio wakimbizi ni dhahiri ambapo wakimbizi wachache ndio wanaandikishwa shuleni, na hivyo kuonesha jinsi kukosa elimu kunawanyima fursa,” amesema Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa UNHCR kwenye utangulizi wa ripoti hiyo. 

Amesema kadri darasa linavyoongezeka, ndivyo fursa ya kuingia sekondari na elimu ya juu inazidi kuwa finyu. 

Bwana Grandi amesema bila fursa za wakimbizi kuongezwa na kupatiwa ufadhili zaidi, wengi wao watabaki nyuma na hivyo kushindwa kukidhi mahitaji yao ya kuondokana na umaskini, kuwa na usawa na ajira. 

Mkitupatia elimu tutaondokana na magumu- Mkimbizi Monicah 

Ripoti ya mwaka huu imepatiwa jina; Kufungua fursa: Haki ya Elim una Fursa, ambapo sio tu inafichua kiwango cha changamozo za elimu kwa wakimbizi, bali pia ustawi wao wanaofikia iwapo wanapata elimu. 

Ripoti imemnukuu Monicah Malith, mkimbizi kutoka Sudan Kusini ambaye sasa anasoma sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi, nchini Kenya akisema “Kwa kutuwezesha kupitia elimu, tunaweza kuvunja mzunguko wa machungu na magumu na kutupatia njia ya kuwa na mustakabali bora.”