Tunachopitia sasa kwenye COVID-19 wahamiaji hupitia kila uchao- Guterres

18 Disemba 2020

Ikiwa leo ni siku ya wahamiaji duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema ni mwaka wa kutathmini jinsi janga la Corona au COVID-19 lilivyosababisha mamilioni ya watu kukumbwa na machungu ya kutengana na familia zao na kutokuwa na uhakika wa ajira, jambo ambalo limewapatia watu hisia halisi ambazo wahamiaji hukumbana nazo kila wakati kwenye maisha yao.
 

Kupitia ujumbe wake, Guterres amesema ni kwa kuzingatia hilo ni lazima kushukuru “utegemezi wetu kwa wale ambao mara nyingi hawaonekani au hawatambuliki katika jamii zetu. Wahamiaji wamekuwa mstari wa mbele na kutekeleza majukumu makubwa katika kukabiliana na janga la sasa. Kuanzia kuhudumia wagonjwa na wazee hadi kuhakikisha vyakula vinapatikana wakati huu wa vizuizi, na hivyo kudhihirisha mchango wao mkubwa katika jamii.”

Katibu Mkuu amesema kama ambavyo wahamiaji ni kiunganishi kikubwa katika jamii, basi wasalie hivyo hivyo wakati wa harakati za kujikwamua

“Lazima tuhakikishe wahamiaji, bila kujali hadhi yao, wanajumuishwa kwenye kila hatua za kukabiliana na janga la Corona, hususan afya na mipango ya chanjo. Lazima tukatae kauli za chuki na vitendo vya chuki dhidi ya wageni,” amesema Guterres.

Wafanyakazi wahamiaji wakiwa kazini katika kiwanda cha matofali huko Mawlamyine, Myanmar.
IOM
Wafanyakazi wahamiaji wakiwa kazini katika kiwanda cha matofali huko Mawlamyine, Myanmar.

Amesema ni lazima kusaka suluhu kwa wahamiaji ambao wamekwama, bila kipato au hadhi ya kihseria, na bila mbinu za kuwawezesha kurejea nyumbani.

Ni kwa mantiki hiyo amesema katika siku hii ya kimataifa ya wahamiaji, “hebu na tutumie fursa hii kujikwamua kutoka kwenye janga na kutekeleza mkataba wa kimataifa wa kuhakikisha uhamiaji salama, wa kisheria na kanuni na kufikiria upya mienendo ya binadamu, na kuwezesha kustawisha uchumi nyumbani na ugenini na kujenga jamii jumuishi na zenye mnepo zaidi.”

IOM nayo yapaza sauti

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, Antonio Vitorino katika ujumbe wake naye pia amemulika suala la wahamiaji na COVID-19.

Amesema kwa mchango wao adhimu katika jamii hivi sasa kiuchumi na kijamii, basi hata katika janga hili la ugonjwa wa corona au COVID-19 wasisaulike kwani nao wana mchango muhimu. 

Bwana Vitorino amesema, “wakati huu chanjo inapatikana, wahamiaji, bila kujali hadhi yao, lazima wahakikishiwe uhakika wa kujumuishwa kwenye mipango ya kitaifa si kama watu maalum bali kama marafiki , majirani na wafanyakazi wenzetu.”

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa hadi mwishoni mwa mwaka 2019, kulikuwepo na wahamiaji milioni 272 ambao ni saw ana asilimia 3.5 ya wakazi wote duniani.
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter