Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa Afrika wapitisha Azimio la Nairobi kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Hali ya hewa na majanga kama mafuriko makubwa, joto na ukame viliathiri mamilioni ya watu na kugharimu mabilioni mwaka 2022, wakati ishara za hadithi na athari za mabadiliko ya hali ya hewa zikiongezeka.
© WMO/Kureng Dapel
Hali ya hewa na majanga kama mafuriko makubwa, joto na ukame viliathiri mamilioni ya watu na kugharimu mabilioni mwaka 2022, wakati ishara za hadithi na athari za mabadiliko ya hali ya hewa zikiongezeka.

Viongozi wa Afrika wapitisha Azimio la Nairobi kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa siku tatu wa viongozi wa Afrika kuhusu tabianchi umekunja jamvi hii leo huko Nairobi Kenya kwa viongozi hao kupitisha Azimio la Nairobi kuhusu mabadiliko ya tabianchi likiwa na vipengele 10 vya hatua za kuchukua ikiwemo wito kwa viongozi wa dunia kutambua kuwa uwepo wa shughuli za kiuchumi zitoazo kiwango kidogo cha hewa ya ukaa, ni fursa pia ya kuchangia katika usawa na ustawi wa watu wote duniani.

Azimio hilo limepitishwa kwa kutambua mambo kadhaa ikiwemo ripoti ya IPCC ya kwamba joto linaongezeka kwa kasi kubwa barani Afrika kuliko mabara mengine na iwapo hatua hazitachukuliwa, mabadiliko ya tabianchi yatakuwa na madhara makubwa kwa uchumi wa Afrika na jamii zake, halikadhalika kukwamisha ukuaji na ustawi wa watu wake.  

Hivyo azimio hilo linakaribisha wadau wa maendeleo kutoka pande zote usaidizi wao wa kiufundi na kifedha kwa Afrika ili kusongesha matumizi endelevu ya maliasili zilizomo kwenye bara hilo ili kutoa kiwango kidogo cha hewa ya ukaa na hivyo kuchangia katika upunguzaji wa hewa hiyo duniani.   

Halikadhalika linataka hatua za kina dhidi ya janga la madeni ili kuepusha nchi kutumbukia kwenye mtego wa kushindwa kulipa na badala yake kuwekwe mfumo unaokidhi mahitaij ya nchi zinazoendelea katika kupata fedha za maendeleo na hatua kwa tabianchi.  

Azimio linapendekeza kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ufadhili unaokidhi mahitaji ya Afrika, ikiwemo marekebisho ya mfumo wa madeni na msamaha kupitia kuanzishwa kwa Chata ya kimataifa ya ufadhili kwa tabianchi kupitia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ifikapo mwaka 2025.  

Pamoja na kuamua kuwa Azimio hili litakuwa msingi wa msimamo wa mchakato wa Afrika kwa tabianchi kuelekea mkutano wa 28 wa mabadiliko ya tabianchi, COP28 baadaye mwaka huu, azimio hilo pia limeitaka Kamisheniya Muunganowa Afrika kuandaa mpango wa utekelezaji na kufanya Mabadiliko ya Tabianchi kuwa maudhumi ya Muungano wa Afrika kwa mwaka 2025 au 2026.  

Mkutano huo wa siku tatu umemazilika leo lakini Wiki ya Tabianchi Afrika iliyoanza tarehe 4 itamalizika tarehe 8 mwezi huu wa Septemba.