Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia wa dhati kuwezesha Afrika kuwa gwiji wa nishati jadidifu duniani- UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia viongozi katika mkutano wa ngazi za juu kuhusu tabianchi barani Afrika unaofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.
UN Photo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia viongozi katika mkutano wa ngazi za juu kuhusu tabianchi barani Afrika unaofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.

Ubia wa dhati kuwezesha Afrika kuwa gwiji wa nishati jadidifu duniani- UN

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa Afrika kuhusu tabianchi ukiingia siku ya pili hii leo huko Nairobi, Kenya, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema nishati jadidifu inaweza kuwa muujiza wa bara la Afrika na kwamba hatua sahihi zikichukuliwa, bara hilo linaweza kuwa kiongozi wa uzalishaji wa nishati hiyo duniani.

Guterres amesema hayo akihutubia viongozi hao akisema Afrika ina asilimia 60 ya vyanzo bora zaidi ya nishati ya sola lakini katika miongo miwili iliyopita imepokea asilimia 2 tu ya uwekezaji wa dunia kwenye vyanzo hivyo.

“Sasa ni wakati wa kuleta pamoja nchi za Afrika, nchi zilizoendelea, taasisi za fedha na kampuni za teknolojia kuunda Ubia wa dhati wa nishati jadidifu Afrika,” amesema Katibu Mkuu.

Makosa ya zamani ya Afrika kuuza malighafi pekee  yasirudiwe

Ameongeza kuwa kukiweko na rasilimali fedha zinazopatikana kwa uhakika na kwa gharama nafuu, halikadhalika usaidizi wa kiteknolojia, nishati jadidifu inaweza kuchochea uchumi, kukuza viwanda, kuanzisha ajira na kuchochea maendeleo, ikiwemo kuwafikia waafrika milioni 600 ambao sasa wanaishi bila nishati ya umeme.

Amefafanua utajiri wa Afrika wa vyanzo vya nishati akisema, bara la Afrika lina asilimilia 30 ya akiba ya madini ambayo ni muhimu katika kuzalisha nishati jadidifu na teknolojia zinazotoa kiwango kidogo cha hewa ya ukaa kama vile nishati ya sola, magari ya kutumia umeme na hifadhi ya betri.

Hata hivyo amesema makosa ya zamani yasirudiwe akimaanisha kwamba pamoja na akiba hiyo ya madini na vyanzo vya nishati jadidifu, “kunufaisha kwa dhati waafrika, lazima uzalishaji na biashara ya madini hayo lazima view endelevu, wazi katika kila mnyororo wa usambazaji na zaidi ya yote viongozewe thamani ndani ya bara la Afrika badala ya kuuzwa kama malighafi.”

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia viongozi katika mkutano wa AFrika kuhusu Tabianchi jijini Nairobi, Kenya.
UN Photo
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia viongozi katika mkutano wa AFrika kuhusu Tabianchi jijini Nairobi, Kenya.

Uongozi Afrika unachochea miradi ya nishati jadidifu

Katibu Mkuu ametumia hotuba yake pia kuangazia jinsi uongozi barani Afrika unavyosaidia kuchochea uchumi bunifu usioharibu mazingira, ukiwa umejikita katika nishati jadidifu.

Kuanzia Pembe ya Afrika ambako asilimia 85 ya umeme unaozalishwa unatokana na nishati jadidifu, ikiwemo miradi mikubwa ya uzalishaji umeme kwa njia ya maji huko Ethiopia, Kenya na Sudan.

Halikadhalika miradi ya kuzalisha umeme kwa njia ya jua na upepo huko Misri, Algeria, Tunisia na Morocco.

“Hadi Msumbiji ambayo inapata takribani asilimia 100 ya umeme wake kutokana na vyanzo visivyoharibu mazingira na endelevu,” amesema Katibu Mkuu akiongezea pia Sudan Kusini ambayo inazidi kusimika miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia sola.

Guterres amesema anashawishika kuwa Afrika inaweza kuwa kitovu cha nishati jadidifu siku za usoni na kwamba “mkutano huu wa viongozi na majawabu yanayodaliwa hapa yanawasilisha hatua kubwa ya kusonga mbele. Lakini hamko peke yenu katika safari hii,” amesema Katibu Mkuu.

Na kwa mantiki hiyo amesema ndio maana mwishoni mwa mwezi huu atakuwa na mkutano wa viongozi kuhusu tabianchi unaolenga kusaka hatua za kimataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na wakati huo huo kusaka usaidizi kwa nchi zinazoendelea wakati huu ziko kwenye kipindi cha mpito kuelekea matumizi ya nishati jadidifu.

Amesema sasa ni wakati kwa nchi zote kusimama kwa pamoja kulinda nyumba yetu pekee. Hebu na tulete haki ya tabianchi kwa waafrika, dunia na sayari wanataka na ni stahili yao.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhutubia viongozi hao, Katibu Mkuu Guterres amesema wakati umefika kuodokana na ukosefu wa haki unaokwamisha bara la Afrika kusonga mbele. Ameahidi kushirikiana na viongozi wa Afrika na mashirika kama vile Muungano wa Afrika ili kusongesha maendeleo hayo.

Mkutano ni wa siku tatu

Mkutano huo wa siku tatu ambao hufanyika kila mwaka, umeandaliwa na sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi UNFCCC, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP, shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira duniani, UNEP, na Benki ya Dunia, kwa msaada wa wadau wa kikanda.

Mkutano huu utakaomalizika kesho Jumatano Septemba 6, unakuja wakati Bara la Afrika linashuhudia kupanda kwa joto kwa kasi zaidi kuliko maeneo mengine duniani, kusababisha matukio ya mara kwa mara ya hali mbaya ya hewa na ukame wa muda mrefu, na kusababisha uhaba wa chakula na watu kupoteza maisha.