Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera ya kuzuia uvutaji sigara hadharini yaleta manufaa kwa umma.

Sera ya kuzuia uvutaji sigara hadharini yaleta manufaa kwa umma.
© Unsplash/Possessed Photograph
Sera ya kuzuia uvutaji sigara hadharini yaleta manufaa kwa umma.

Sera ya kuzuia uvutaji sigara hadharini yaleta manufaa kwa umma.

Afya

Miaka 15 baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO kuanzisha sera ya kulinda umma kutoathirika na uvutaji wa sigara unaofanywa na mtu mwingine, zaidi ya watu bilioni 5.6 wamenufaika na sera hiyo ulimwenguni kote, imesema ripoti mpya ya shirika hilo iliyotolewa leo. 

Idadi hiyo ni sawa na kusema kuwa asilimia 71 ya watu ulimwengu kote sasa wamelindwa na athari ambazo wangeweza kuzipata kutokana na mtu mwingine kuvuta sigara karibu yake. Na iwapo kusingekuwa na sera hizo zaidi ya watu milioni 300 wangekuwa wametumbukia katika uvutaji moshi wa sigara bila wao kuvuta wenyewe.

Akizindua ripoti hiyo ya  9  ya janga la uvutaji tumbaku ulimwengu hii leo jijini Geneva Uswisi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema mikakati 6 iliyopendekezwa kuwa sera imeanza kuleta mafanikio ambapo watu 7 kati ya 10 ulimwenguni wanalindwa na angalau Sera moja. 

Dkt. Tedros amesema “takwimu hizi zinaonesha japo ni polepole lakini kwa hakika, watu wengi zaidi wanalindwa dhidi ya madhara ya tumbaku kwa kutumia sera za utendaji bora za WHO zilizotungwa kwa msingi wa ushahidi.”

Matumizi ya tumbaku ni moja ya sababu kuu ya vifo vinavyoweza kuzuiwa.
Unsplash/Lex Guerra
Matumizi ya tumbaku ni moja ya sababu kuu ya vifo vinavyoweza kuzuiwa.

Fahamu sera za MPOWER

Sera hizo ziitwazo MPOWER zinataka serikali kuweka mikakati sita ya kudhibiti tumbaku ambayo ni 

Mosi; Fuatilia sera za matumizi na uzuiaji wa tumbaku, Pili; kuweka kinga ya kulinda watu dhidi ya moshi wa tumbaku, Tatu; kutoa usaidizi wa wale wanaotaka kuacha matumizi ya tumbaku; Nne,kuelimisha watu kuhusu hatari za tumbaku, Tano; kuweka marufuku ya utangazaji, ukuzaji na udhamini wa bidhaa za tumbaku na sita; kuongeza ushuru kwa bidhaa za tumbaku.

Heko Mauritius na Uholanzi

Nchi za Brazil na Uturuki zilifanikiwa kutekeleza sera hizo kwa viwango vya juu na leo Mkuu huyo wa WHO amezipongeza nchi ya Mauritius kwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika, na Uholanzi kwa kuwa ya kwanza katika Muungano wa Ulaya kutekeleza mpango kamili wa sera hizo za kudhibiti matumizi ya tumbaku.

WHO pia imeeleza ipo tayari kuunga mkono nchi zote kufuata mfano wao na kuwalinda watu wao kutokana na janga hili baya.