Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utalii warejea kwa kasi Afrika baada ya kutwamishwa na COVID-19- UNWTO

Tembo wa Kiafrika katika Hifadhi ya Kitaifa ya Maasai Mara, Kenya. Licha ya kuongezeka kwa ujangili katika sehemu nyingi za Afrika, idadi ya tembo huko Mara inaongezeka kwa sasa.
Photo: UNEP GRID Arendal/Peter Prokosch
Tembo wa Kiafrika katika Hifadhi ya Kitaifa ya Maasai Mara, Kenya. Licha ya kuongezeka kwa ujangili katika sehemu nyingi za Afrika, idadi ya tembo huko Mara inaongezeka kwa sasa.

Utalii warejea kwa kasi Afrika baada ya kutwamishwa na COVID-19- UNWTO

Ukuaji wa Kiuchumi

Takwimu mpya za shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii duniani, UNTWO zinaonesha kuwa utalii barani Afrika umeanza kurejea kwa kasi kubwa baada ya kutwama wakati wa janga la COVID-19.

Takwimu hizo zimetolewa kwenye mkutano wa 66 wa Kamisheni  ya UNWTO kwa Afrika unaoendelea huko Mauritius ukifanya tafakuri ya kuimarisha mchango wa sekta hiyo kama kichocheo cha maendeleo barani humo. 

Washiriki wa mkutano huo wa siku tatu ambao leo umeingia siku ya pili wamearifiwa kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2023 idadi ya watalii wa kigeni wanaowasili barani Afrika sasa ni asilimia 88 kulinganisha na kabla ya janga la coronavirus">COVID-19 mwaka 2019, Morocco na Mauritius wakiwa  ‘kidedea.’ 

Kikanda, eneo la Afrika Kaskazini ndio limeshamiri zaidi kitalii ambapo idadi ya watalii wa nje katika robo ya kwanza ya mwezi huu iliongezeka kwa asilimia 4 zaidi kulinganisha na kipindi kama  hicho kabla ya COVID-19.  

Ajenda ya UNWTO kwa Afrika imeridhiwa 

Katibu Mkuu wa UNWTO Zurab Pololikashvili akizungumza kwenye mkutano  huo amesema ajenda ya UNWTO kuhusu Afrika imeridhiwa na kwamba dira yetu kwa utalii Afrika ni dira ambayo pia inalenga kuona utawala thabiti, elimu zaidi na ajira bora na nyingi zaidi kwenye sekta hiyo.  

Ili kufanikisha hilo amesema “tunalenga kuhamasisha na kuendeleza ugunduzi, uchechemuzi juu ya kuitangaza Afrika, kufanikisha safari na kufungua ukuaji kupitia  uwekezaji na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.” 

Mkutano huo  unaohudhuriwa na wawakilishi wa serikali wa nchi wanachama wa UNWTO, mashirika ya  kimataifa, wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii, utamalizika tarehe 28 Julai 2023.