Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFSS+2 yahitimishwa huko Roma viongozi waeleza mwelekeo

Naibu Katibu Mkuu Amina Mohammed akihutubia wakati wa kufunga Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mifumo ya Chakula +2  mjini Rome, Italia.
FAO/Alessandra Benedetti
Naibu Katibu Mkuu Amina Mohammed akihutubia wakati wa kufunga Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mifumo ya Chakula +2 mjini Rome, Italia.

UNFSS+2 yahitimishwa huko Roma viongozi waeleza mwelekeo

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mifumo ya Chakula +2 (UNFSS+2) umefikia tamati leo Jumatano katika makao makuu ya  Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) baada ya siku tatu vikao vya ngazi ya juu, mikutano na midahalo iliyowaleta Pamoja mjini Roma, Italia washiriki zaidi ya 2000 kutoka nchi 180, wakiwemo zaidi ya Wakuu 20 wa Nchi na Serikali na Mawaziri 125, ili kuchunguza changamoto na fursa za kubadilisha mifumo ya kilimo cha chakula. 

Katika hotuba yake ya kufunga, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu, amesema anatumai washiriki wameondoka Roma na mambo muhimu ya kuchukua ili kusaidia njia zao za kitaifa, baada ya kutambua kwa pamoja kwamba vichochezi vya uhaba wa chakula na utapiamlo vimezidi kuwa vigumu zaidi kutokana na kuimarika na kuunganishwa kwa hatari na athari za janga la tabianchi, mitikisiko ya kiuchumi na mizozo inayoendelea. 

Mkurugenzi Mkuu wa FAO ametambua mijadala kuhusu hitaji la dhamira ya juu ya kisiasa ya muda mrefu na akasisitiza kuwa kubadilisha mifumo ya kilimo cha chakula ni muhimu ili kufikia uhakika wa chakula. 

"Katika ulimwengu ambapo makadirio yanaonesha watu milioni 600 watakuwa na njaa ifikapo mwaka 2030, kubadilisha mifumo ya chakula cha kilimo duniani sio chaguo, ni lazima kuhakikisha uhakika wa chakula kwa wote. Natumai Kipindi hiki kimetoa dirisha kamili la kuona tunasimama wapi, tumefanya nini hadi sasa, na ni kiasi gani tunahitaji kufanya zaidi na bora zaidi. Njia ni ndefu na tunahitaji kuharakisha hatua yetu.” Amesema QU 

QU amesisitiza kuwa FAO imejitolea kusaidia wanachama pamoja na njia zao za kitaifa kuelekea uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora, na maisha bora, bila kuacha mtu nyuma. 

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, akifunga rasmi UNFSS+2 kwa kusoma Wito wa Kuchukua Hatua kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amependekeza hatua za haraka zichukuliwe ili kuziba pengo la utekelezaji, akiangazia uhusiano wa kufadhili maendeleo, msamaha wa madeni, na upatikanaji wa sayansi, teknolojia na uvumbuzi kwa wote. Pia alielezea vipaumbele muhimu kwa hatua zaidi za watendaji wa serikali na wasio wa serikali. 

"Katika kila hatua, Mfumo wa Umoja wa Mataifa, ukiongozwa na hatua iliyoratibiwa ya mashirika yenye makao yake makuu mjini Rome FAO, WFP na IFAD, na Kituo cha Uratibu wa Mifumo ya Chakula cha Umoja wa Mataifa, utaendelea kutoa uongozi ili kufanya mabadiliko ya mifumo ya chakula kuwa ukweli kwa nchi 155 na wadau ambao tayari wameanza mchakato huu, na wale ambao tunahimiza kujiunga nao katika siku zijazo. Ni jukumu letu la pamoja na madhumuni yetu ya pamoja. Tunajivunia kuchukua safari hii pamoja nanyi nyote. Wacha tuchukue ari ya kukusanyika huku katika msukumo mpana wa kuokoa SDGs na katika juhudi madhubuti za kila siku za kufanya mifumo ya chakula kufanya kazi kwa kila mtu.” Amesema Amina Mohammed. 

Hafla ya kufunga pia imemshirikisha Rais wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Alvaro Lario, na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Cindy McCain. 

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mifumo ya Chakula +2 umejengwa juu ya kasi ya Mkutano wa Kilele wa Mifumo ya Chakula wa 2021 kwa kuunda nafasi mwafaka kwa nchi kukagua maendeleo ya ahadi za kuchukua hatua na kutambua mafanikio, vikwazo na vipaumbele vinavyostahimili. 

Tukio hilo la siku tatu la ngazi ya juu liliitishwa na Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa na kuandaliwa na Italia, kwa ushirikiano na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake makuu mjini Roma, (FAO), (IFAD), na (WFP). 

Mkutano wa Mifumo ya Chakula unaofuata, utafanyika mwaka 2025.