Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kupitia uwezo wa kidijitali Kiswahili chaweza kuwa mkombozi wa kiuchumi pia: Wadau

Ukumbi wa mikutano wa Umoja wa Mataifa katika maadhimisho ya siku ya Lugha ya Kiswahili
UN News
Ukumbi wa mikutano wa Umoja wa Mataifa katika maadhimisho ya siku ya Lugha ya Kiswahili

Kupitia uwezo wa kidijitali Kiswahili chaweza kuwa mkombozi wa kiuchumi pia: Wadau

Utamaduni na Elimu

Katika ukumbi wa mikutano wa Umoja wa Mataifa namba 4 pilika na hekaheka ni nyingi wadau mbalimbali wamekusanjika kuadhimisha siku hii adhimu ya lugha ya Kiswahili duniani

Hafla imefunguliwa na waziri wa elimu na mafunzo ya amali wa Zanzibar Tanzania Lela Mohamed Mussa na baada ya kuwakaribisha wageni ambao wanajumusiha mabalozi wa kudumu w anchi mbalimbali kwenye umoja wa Mataifa, wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, taasisi mbalimbali, wanazuoni  na wapenzi wa kiswahili akasema, “Maadhimisho haya yanatukumbusha kutambua na kuthamini nafasi ya lugha hiyo na utamaduni wake katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi duniani, uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa hasa za sanaa na za kiutamaduni, ni rasilimali muhimu zinazoweza kutumiwa pamoja na lugha ili kuleta maendeleo ya lugha na wananchi wa mataifa mbalimbali duniani."

Maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani katika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.
UN News Kiswahili
Maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani katika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.

UNESCO ndio waliohakikisha kuwepo kwa siku hii , katika ujumbe wake wa mwaka huu mkurugenzi mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema “Kiswahili hakisimulii tu hadithi ya mazungumzo kati ya lugha, bali pia mazungumzo kati ya watu na nchi. Kwa hakika, kwa sababu Kiswahili hushiriki maneno na dhana na lugha nyingine za Kiafrika, kina nguvu ya kuvutia ya kuunganisha watu.”

Maudhi ya mwaka huu ni ‘Kuibua uwezo wa Kiswahili katika zama za kidijitali“ Bi. Azoulay amesema “Ndio maana UNESCO imejitolea kuhakikisha kwamba uwezo wa Kiswahili pia unatimizwa mtandaoni, na kwa nini, katika juhudi zetu za kubuni miongozo ya udhibiti wa mifumo ya kidijitali, tunaangazia umuhimu wa kuwepo kwa lugha mbalimbali katika kusawazisha maudhui, ili kukabiliana vyema na kauli za chuki na habari potofu, huku tukikuza uhuru wa kujieleza na haki za binadamu.”

Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye hafla hii umewasilishwa na Maheri Nassir mkurugenzi wa kitengo cha ufikiaji wa wadau katika Idara ya mawasiliano ya kimataifa DGC.

Naye mgeni rasmi wa hafla hii Dkt. Ida Hadjivayanis mtafsiri na mhadhiri kutoka chuo kikuu cha SOAS jijini  London Uingereza amesema, “Kiswahili si njia ya mawasiliano tu bali ni mfumo mzima wa mawazo, itikadi, falsafa na tamaduni ambazo zimekuwa zikikua kwa karne nyingi. Kiswahili kilienea kutokana na biashara na kushirikiana kwa jamii tofauti; biashara zilizohusisha nchi zinazoguswa na Bahari ya Hindi kuanzia mwambao wake kuelekea bara zima la Afrika Mashariki na Kati, sehemu za ughaibuni kama Uajemi, nchi za Kiarabu, Bara Hindi, Australia na hata Uchina.”

Mgeni rasmi wa hafla ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani Dkt. Ida Hadjivayanis, ambaye ni Mtafsiri na Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha SOAS jijini  London Uingereza.
UN News
Mgeni rasmi wa hafla ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani Dkt. Ida Hadjivayanis, ambaye ni Mtafsiri na Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha SOAS jijini London Uingereza.

Na kuhusu suala la Kiswahili katika zama za kidijitali amesema kuna hatua zinapigwa lakini  “Hata hivyo, kuna umuhimu wa kukiri kwamba bado kuna mgawanyiko wa kidijitali usio na usawa katika bara la Afrika. Kuna tofauti katika upatikanaji wa mtandao, ujuzi wa kidijitali, na miundombinu ya kiteknolojia kati ya maeneo ya mijini na vijijini, na pia katika nchi mbalimbali. Juhudi zinafanywa ili kuziba mapengo haya kupitia mipango inayokuza mafunzo ya ujuzi wa kidijitali, kupanua muunganisho, na kuwekeza katika miundombinu ya kiteknolojia."

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba, “Tukumbuke tu kwamba, kukikumbatia Kiswahili katika enzi ya kidijitali sio tu suala la kuhifadhi lugha; ni fursa ya kuwawezesha watu, kuimarisha jamii, na kuendesha ukuaji wa uchumi. Tumeutambua uwezo mkubwa wa Kiswahili, sasa tushirikiane kwa pamoja, katika tofauti zetu, ili kuhakikisha kwamba lugha hii inachukua nafasi yake ipasavyo katika mapinduzi ya kidijitali. Kwa pamoja, tunaweza kutengeneza mustakabali mwema kwa wote wanaoithamini lugha hii adhimu.”

Hafla hii inaambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo mijadala, burudani na hata vyakula vya kiswahili. Basi nami nakutakia kila la heri katika kukienzi na kukiendeleza  Kiswahili.