Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO imedhamiria kuhahakikisha uwezo wa Kiswahili unatamalaki pia mtandaoni: Azoulay

Audrey Azoulay mkurugenzi mkuu wa UNESCO
UNESCO
Audrey Azoulay mkurugenzi mkuu wa UNESCO

UNESCO imedhamiria kuhahakikisha uwezo wa Kiswahili unatamalaki pia mtandaoni: Azoulay

Utamaduni na Elimu

Leo ni siku ya lugha ya Kiswahili duniani ambayo kila mwaka tangu kutangazwa rasmi mwaka 2021 inaadhimishwa Julai 7.

Katika ujumbe wake wa siku hii iliyobeba maudhui “kuibua uwezi wa Kiswahili katika zama za kidijitali” mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO Audrey Azoulay amesema “Kiswahili ni lugha inayozungumza na watu wa zamani na wa sasa. Ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200, ni mojawapo ya lugha za Kiafrika zinazotumiwa sana, ikijumuisha lahaja zaidi ya kumi na mbili kuu. Kwa karne nyingi, lugha hii ya Kibantu imeibuka kama njia ya kawaida ya mawasiliano katika maeneo mengi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, pamoja na Mashariki ya Kati.”

Bi. Azoulay ameendelea kusema kwamba Kiswahili kama lugha iliyokumbatiwa na wengi wanaozungumza lugha tofauti kuwa lugha ya Pamoja au lingua franka, pia kimejumuisha maneno kutoka lugha nyingine, hasa Kiarabu, huku kikiboresha lugha hizi kama fidia.

Kwa mfano, amesema neno la Kiingereza “safari” linatokana na neno la Kiswahili la “safari”, ambalo asili yake ni kitenzi cha Kiarabu cha “safari”, safara. Mabadilishano haya ya kiisimu yanaangazia dhima muhimu ya Kiswahili katika muingiliano wa lugha za ulimwengu.

Miongoni mwa washiriki wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani kwenye makao makuu ya UN,  New York, Marekani. Mwaka 2021 UNESCO ilitangaza Julai 7 kuwa siku ya Kiswahili duniani
UN /Manuel Elias
Miongoni mwa washiriki wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani. Mwaka 2021 UNESCO ilitangaza Julai 7 kuwa siku ya Kiswahili duniani

Kiswahili ni zaidi ya mawasiliano ya lugha

Ujumbe wa mkuu huyo wa UNESCO umeendelea kusema kwamba “Kiswahili hakisimulii tu hadithi ya mazungumzo kati ya lugha, bali pia mazungumzo kati ya watu na nchi. Kwa hakika, kwa sababu Kiswahili hushiriki maneno na dhana na lugha nyingine za Kiafrika, kina nguvu ya kuvutia ya kuunganisha watu.”

Ameongeza kuwa ndio maana Muungano wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC zote zimechagua Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha zao rasmi. 

“Kwa njia hii, Kiswahili kitakuwa na jukumu la kuhakikisha bara la Afrika linafikia uwezo wake kamili lengo ambalo UNESCO pia inalishughulikia, kupitia kipaumbele cha kimataifa cha Afrika.”

Amesisitiza kuwa mbali ya kuwa lugha ya biashara, diplomasia na Uumoja “Kiswahili ni chanzo kikubwa cha kujieleza kitamaduni.”

Kwa maana amesema inajumuisha dhana kama vile amani, tamko la kawaida katika mwingiliano wa kila siku. 

“Amani haieleweki tu kama kutokuwepo kwa migogoro, lakini pia kama hali ya utulivu au ukimya. Kwa hivyo, ni jambo la kuendelea kufanyia kazi maono ambayo yanahusiana na dhana ya UNESCO ya amani kama njia bora ambayo tunaipigania.”

Amesisitiza kwamba “Nguvu hii ya kukuza mawasiliano na amani lazima ilindwe  hasa katika kukabiliana na mapinduzi ya kidijitali.”

Kamusi ya Kiswahili toleo la 3 ilizinduliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Dr.phillip Mpango kwenye Kongamano la dunia la Kiswahili
UN/ Stella Vuzo
Kamusi ya Kiswahili toleo la 3 ilizinduliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania Dr.phillip Mpango kwenye Kongamano la dunia la Kiswahili

UNESCO imedhamiria kutimiza ndoto za Kiswahili

Azoulay amesema “Ndio maana UNESCO imejitolea kuhakikisha kwamba uwezo wa Kiswahili pia unatimizwa mtandaoni, na kwa nini, katika juhudi zetu za kubuni miongozo ya udhibiti wa mifumo ya kidijitali, tunaangazia umuhimu wa kuwepo kwa lugha mbalimbali katika kusawazisha maudhui, ili kukabiliana vyema na kauli za chuki na habari potofu, huku tukikuza uhuru wa kujieleza na haki za binadamu.”

Amehitimisha ujumbe wake kwa wito kwamba “Katika Siku hii, hebu tusherehekee urithi wa lugha na utajiri wa kitamaduni unaoenezwa la lugha.

Wacha tujitolee kulinda wingi na utofauti wa lugha ili kuelezea maadili na maono yetu ya ulimwengu kwa kiwango cha kibinafsi, kukuza amani na kuwezesha ushirikiano katika kiwango cha kijamii. Heri ya Siku ya Lugha ya Kiswahili duniani”