Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa watumishi wa umma ni muhimu katika kujenga mustakbali bora kwa wote: Guterres

Mhudumu wa afya nchini Malawi akipatia mtoto matone ya vitamin A.
© UNICEF Malawi
Mhudumu wa afya nchini Malawi akipatia mtoto matone ya vitamin A.

Mchango wa watumishi wa umma ni muhimu katika kujenga mustakbali bora kwa wote: Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo ni siku ya Umoja wa Mataifa ya watumishi wa umma, ambapo katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema mchango wao ni muhimu sana katika ufanikishaji wa malengo ya maendeleo endelevu na kuhakikisha mustakbali bora kwa wote.

Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii amesema lengo lake ni kuwaenzi wanawake na wanaume kote duniani ambao huwajibika kwa jukumu muhimu zaidi la kutoa huduma kwa umaa.

Amesema maadhimisho ya siku ya mwaka huu yanakuja wakati Dunia iko katikati ya  kuelekea ukomo wa ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu na hivyo amesisitiza kuwa “ Watumishi wa umma na taasisi wanazoziunga mkono zitakuwa muhimu zaidi huku ulimwengu ukiharakisha hatua za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, ambayo yako yanakwenda kombo.”

Ameichagiza dunia kwamba ili kutimiza malengo hayo “ Teknolojia lazima iwe kiini cha kuongeza kasi hii ya utekelezaji. Kila siku, teknolojia mpya zinaibuka ambazo zinashikilia uwezo wa kubadilisha jinsi tunavyoishi na kufanya kazi. Inapotumiwa na utumishi wa umma wenye ujuzi, uliowezeshwa na wenye vifaa, teknolojia inaweza kuboresha ufikiaji na ufanisi wa huduma za umma, huku ikisukuma maendeleo kuelekea utimizaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.”

Amehitimisha ujumbe wake kwa wito kwamba “Wakati tukiadimisha siku hii muhimu hebu tusherehekee sio tu kazi ya utumishi wa umma kote duniani lakini tutafute njia mpya za kutumia ubunifu katika kazi zetu na kuenzi uwajibikaji wa watumishi hao wa kufanyakazi kwa ushirikiano ili kujenga mustakbali bora kwa watu wote.”