Leo ni siku ya kimataifa ya mwezi
Leo ni siku ya kimataifa ya mwezi
Leo ni siku ya kimataifa ya mwezi ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza siku hii ya kimataifa iliyoteuliwa na Umoja wa Mataifa kuadhimishwa kila mwaka tarehe 20 Julai, katika azimio lake nambari 76/76 kuhusu "Ushirikiano wa Kimataifa katika matumizi ya amani ya anga za mbali" mwaka 2021.
Kwa nini Siku ya Mwezi?
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa siku ya kimataifa ya mwezi huadhimisha kumbukumbu ya kutua kwa mara ya kwanza kwa wanadamu kwenye mwezi kama sehemu ya operesheni ya Apollo 11.
Maadhimisho ya siku hii pia yanazingatia mafanikio ya mataifa yote katika uchunguzi wa Mwezi na kuongeza ufahamu kwa umma kuhusu uchunguzi na matumizi endelevu ya mwezi.
Historia fupi
Kwa maelfu ya miaka, ustaarabu wa binadamu umekuwa ukitazama juu angani na kutafakari asili na mafumbo ya mwezi ambao ni satelaiti yetu ya kipekee ya asili. Uchunguzi wa msingi uliowezeshwa na uvumbuzi wa darubini za kwanza ulifungua sura mpya katika ufahamu wetu wa mwenzetu wa angani.
Pamoja na kuzaliwa kwa shughuli za anga, mwezi ukawa mahali pa mwisho pa operesheni nyingi, zikijumuisha ndege za wafanyakazi ambazo ziliacha nyayo za kwanza za binadamu mahali pengine katika ulimwengu.
Juhudi za uchunguzi wa mwezi zinapoendelea kuchukua sura na mipango kabambe, maadhimisho haya ya kimataifa yanatumika sio tu kama ukumbusho wa mafanikio ya zamani, lakini kama ushuhuda wa kila mwaka wa juhudi za siku za usoni.
UN na masuala ya anga
Tangu mwanzo kabisa wa enzi ya anga, Umoja wa Mataifa ulitambua kwamba anga za juu ziliongeza mwelekeo mpya wa kuwepo kwa wanadamu.
Familia ya Umoja wa Mataifa inajitahidi kuendelea kutumia manufaa ya kipekee ya anga za juu kwa ajili ya kuboresha wanadamu wote.
Kwa kutambua maslahi ya pamoja ya wanadamu katika anga za juu na kutaka kujibu maswali kuhusu jinsi anga za juu zinavyoweza kusaidia watu wa dunia, Baraza Kuu lilipitisha azimio lake la kwanza kuhusiana na anga za juu, azimio namba 1348 (XIII) lenye kichwa "Swala la matumizi ya amani ya anga za Juu".
Mkataba wa anga za juu
Tarehe 10 Oktoba mwaka 1967, mkataba wa "Magna Carta of Space", ambao pia unajulikana kama “Mkataba wa Kanuni zinazosimamia shughuli za mataifa katika uchunguzi na matumizi ya anga, ikiwa ni pamoja na mwezi na vinginevyo vya angani” ulianza kutumika.
Leo hii ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya anga za juu (UNOOSA) ni ofisi inayohusika na kukuza ushirikiano wa kimataifa katika matumizi ya amani ya anga za juu.
UNOOSA inatumika kama sekretarieti ya kamati pekee ya Baraza Kuu inayoshughulikia ushirikiano wa kimataifa katika matumizi ya amani ya anga za juu: Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Matumizi ya Amani ya Anga za Juu (COPUOS).
UNOOSA pia ina jukumu la kutekeleza majukumu ya Katibu Mkuu chini ya sheria ya kimataifa ya anga na kudumisha daftari la Umoja wa Mataifa la vitu vilivyozinduliwa angani.