Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Wakimbizi Duniani, wakimbizi wa ndani DRC wanasemaje?

Watoto wakiteka maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani, Rusayo, DRC.
George Musubao
Watoto wakiteka maji katika kambi ya wakimbizi wa ndani, Rusayo, DRC.

Siku ya Wakimbizi Duniani, wakimbizi wa ndani DRC wanasemaje?

Wahamiaji na Wakimbizi

Hapa ni kambi ya wakimbizi wa ndani ya Rusayo iliyoko takribani kilometa 17 magharibi mwa mji wa Goma, jimboni Kivu kaskazini, Mashariki mwa DRC, ndivyo anavyoanza kusimulia George Musubao, Mwandishi wa Habari wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa nchini DRC aliyesafiri kutoka Beni hadi kambini Rusayo kuzungumza na wananchi ambao wamelazimika kukimbia makazi yao na sasa maisha yao yanategemea hisani za jumuiya ya kimataifa kupitia Umoja wa Mataifa. 

"Napatikana kwenye kambi hii ya Rusayo nikiwa mkimbizi kutokea Mweso wakati ya vita ya M23.” Huyu ni Tauchi Cecile Vitsura mmoja wa wakimbizi wa ndani wanaohifadhiwa hapa katika kambi ya Rusayo jimboni Kivu kaskazini. Tauchi anaendelea kueleza hali ilivyokuwa akisema,“Vita ilikua kubwa ngambo ya Rutsuru, tuliona watu wakikimbia kutoka Kitchana wakafika Mweso. Mlipuko wa mabomu ulisikika sana ndivyo sisi pia tukakimbia kwenda ngambo za Masisi tukapita huko Mushaki mpaka hapa kwenye Kambi ya Rusayo". 

Taushi Cécile anashuhudia ya kwamba bila Umoja wa Mataifa kuwasaidia wakimbizi mambo yangekuwa mabaya zaidi na hatari kwa maisha yao,"Umoja wa ma Mataifa wametusaidia sana. Kupitia WFP wametupatia chakula, ila si watu wote. Wanasaidia wakambizi kwenye kambi iliyo ngambo ya Bulengo, kambi hiyo ilikua pembeni ya Ziwa Kivu ambamo mna gesi methene iliYokuwa inasababisha vifo vya wakimbizi wengi. Kwa sasa Umoja wa Mataifa wametujengea nyumba. Ingawa bado hazitoshi ila wamesaidia sana. Tuna imani kwamba wataendelea kuwapa chakula wakimbizi waliokua huko Bulengo. Kambi ya Rusayo 1 na Rusayo 2 tumekuwa pamoja. Tuko hapa katika hali ya ukimbizi, ni hali ya changamoto." 

Kwa upande wake, Zainabo Simire naye pia mkimbizi katika kambi hii hii ya Rusayo anatoa shukrani na pia wito kwa Umoja wa Mataifa akisema,"Nina furaha sana kuona Umoja wa Mataifa umetujengea nyumba. Tulikua tukiteseka ila tumeanza kulala vizuri tunapata chakula kama inavyofaa. Umoja wa Mataifa Mungu awabariki. Nawaomba zaidi ya hiyo waendelee kutusaidia kupitia miradi mingine." 

Cecile Vitsura akijibu swali anadhani maisha ya wakimbizi yangekuwaje kama mashirika ya Umoja wa Mataifa yasingekuwepo? anasema,"Umoja wa Mataifa uko na kazi inayofaa wametusaidia sana. Pasipo Umoja wa Mataifa hatungelipata maji, hatungelipata vyoo, chakula na hata nyumba. Wamejitolea kutuletea misaada hiyo. Zaidi ya haya wameweka hapa askari polisi wanaofanya ulinzi wa kambi Rusayo" 

Pamoja na misaada hiyo ambayo wakimbizi wa ndani wanaipata lakini bado changamoto kadha wa kadha zipo na kwa hiyo bado wanahitaji usaidizi kuongezeka. Wakimbizi hawa wanazitaja baadhi ya changamoto hizo. Lukoo Kitsa Catherine anasema,"Shida tuliyonayo ni kwamba tuna teseka na njaa. Baadhi walipokea chakula lakini sisi bado hatujapokea. Kuna ugonjwa wa Kipindupindu unaoua watoto, wengine wanalala bila kula hadi wengine wanakufa na njaa. Sasa tunaomba viongozi wa DRC na Umoja wa Mataifa wasilishe mtoto mmoja nakuacha mwingine. Tulikimbia hatuna nguo pia na vyombo vya kupikia chakula” 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu Misaada ya dharura OCHA imetangaza kwamba tangu mwanzoni mwa mwaka huu 2023, karibu watu takriban 677,000 wamekua wakimbizi nchini DRC. Hesabu hiyo imefanya jumla waliokimbia makazi nchini humu kufikia milioni 6. Wanawake wanawakilisha asilimia hamsini na moja ya watu waliokimbia maeneo yao. Zaidi ya asilimia tisini na nne ya watu waliokimbia maeneo yao ni kutokana na mashambulizi na mapigano ya makundi yenye silaha. 

Taarifa hii imeandaliwa na George Musubao, DRC.