Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutumia ukatili wa kingono kama silaha ya vita lazima kukome: Guterres

Jane (si jina lake halisi) ni manusura wa ukatili wa kingono.
UNICEF/Zahara Abdul
Jane (si jina lake halisi) ni manusura wa ukatili wa kingono.

Kutumia ukatili wa kingono kama silaha ya vita lazima kukome: Guterres

Amani na Usalama

Matumizi ya unyanyasaji wa kingono kama mbinu ya vita, mateso na ukandamizaji yameenea katika migogoro inayoathiri mamia ya mamilioni ya watu duniani kote amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kingono katika mizozo.

Guterres amesema “Ripoti za kutisha kutoka kote ulimwenguni ni ukumbusho mbaya kwamba uhalifu huu wa kuchukiza unaendelea licha ya ahadi za kimataifa za kuukomesha. Na wengi wa wale wanaohusika kamwe hawakabiliani na mkono wa sheria. Wakati unyanyapaa mara nyingi husababisha waathirika kutembea kwa aibu, wahalifu hutembea huru.”

Guterres ameongeza kwamba “Leo, katika Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Unyanyasaji wa kingono katika migogoro, tunasimama kwa mshikamano na manusura na kila mtu anayewaunga mkono. Na tunajitolea kuongeza juhudi zetu ili kuzuia ukatili huu na kuwawajibisha wale wanaohusika.”

Robo ya visa vya ukatili wa kingono nchini Sudan Kusini ni dhidi ya watoto.
© UNICEF/Mackenzie Knowles-Coursin
Robo ya visa vya ukatili wa kingono nchini Sudan Kusini ni dhidi ya watoto.

Lazima tuwasikilize waathirika

Katibu Mkuu amesema “Hiyo ina maana kuwasikiliza waathirika, inamaanisha kuwa na serikali zinazojumuisha sheria za kimataifa za kibinadamu katika sheria za kitaifa, kanuni za kijeshi na mafunzo na inamaanisha kuwawajibisha wahalifu, ili wakabiliane na haki lazima tukabiliane na imani kwamba wapiganaji wanaweza kuleta hofu na kutekeleza uhalifu bila kuadhibiwa.”

Siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kingono katika migogoro mwaka huu inaangazia teknolojia na mgawanyiko wa kidijitali. 

Guterres amesema teknolojia inayoweza kufikiwa inaweza kuwaonya watu kuhusu hatari, kuwasaidia kufika mahali salama na kupata msaada, na kuwezesha matumizi mabaya kurekodiwa na kuthibitishwa, kama hatua ya kwanza kuelekea uwajibikaji. 

Lakini pia amesema teknolojia inaweza kuendeleza vurugu, kuwadhuru waathirika na kuwasha moto wa chuki. 

Kwa mantiki hiyo amesisitiza “Ni lazima tuhakikishe teknolojia inaunga mkono juhudi zetu za kuzuia na kukomesha uhalifu huu, ikiwa ni pamoja na kuongeza fursa za ufikiaji wa intaneti na kuwawajibisha watu kwa matendo yao mtandaoni. Kwa pamoja, lazima tugeuze kauli kuwa vitendo, na ahadi kuwa vitendo, ili kufanya ahadi za kukomesha unyanyasaji wa kingono katika migogoro kutimia.”