Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urusi yakataa maeneo wanayoshikilia kupelekwa msaada wa kibinadamu

© UNICEF Ukraine
Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wa kibinadamu wanaendelea kuunga mkono mahitaji ya dharura ya walioathiriwa na mafuriko.
© UNICEF Ukraine

Urusi yakataa maeneo wanayoshikilia kupelekwa msaada wa kibinadamu

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa umekuwa ukishirikiana na Serikali za Ukraine na Urusi kuhusu utoaji bora wa misaada ya kibinadamu kwa watu wote walioathiriwa na uharibifu mkubwa wa Bwawa la Kakhovka.

Mratibu mkazi wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine Denise Brown katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu maendeleo ya utoaji wa misaada amesema mpaka sasa “nchi ya Urusi imekataa ombi letu la kufikia maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake wa kijeshi wa muda.”

Bi Brown ameeleza Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na kila mdau ili kutafuta ufikiaji unaohitajika kwa watu wenye uhiyaji.

Hata hivyo ameisihi mamlaka ya Urusi “kuchukua hatua kulingana na majukumu yao kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu kwani msaada hauwezi kukataliwa kwa watu wanaohitaji. “

Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kila uwezalo kuwafikia watu wote - ikiwa ni pamoja na wale wanaoteseka kutokana na uharibifu wa hivi karibuni wa mabwawa - ambao wanahitaji haraka msaada wa kuokoa maisha, bila kujali wapi walipo.