Jumla ya dola bilioni 2.4 zachangwa kusaidia wakazi wa Pembe ya Afrika
Jumla ya dola bilioni 2.4 zachangwa kusaidia wakazi wa Pembe ya Afrika
Nuru ya usaidizi kwa wakazi wa Pembe ya Afrika wanaogubikwa na majanga ya njaa, ukosefu wa usalama na mabadiliko ya tabianchi inaanza kuonekana baada ya wahisani hii leo kutangaza jumla ya dola bilioni 2.4 kusaidia wananchi hao.
Fedha hizo zimepatikana wakati kwenye tukio lililofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, na walengwa ni takribani watu milioni 32 walioko Ethiopia, Kenya na Somalia.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA mwishoni mwa mkutano huo imemnukuu Naibu Mkuu wa ofisi hiyo Joyce Msuya akiasema “tunakaribisha matangazo ya leo ya usaidizi kwa watu wa Pembe ya Afrika, ambao wanahitaji ahadi yetu endelevu ili wajikwamue kutoka kwenye janga lenye msururu wa maangamizi.”
Amesema ni lazima kuendelea kushinikiza uwekezaji hasa katika kujenga uwezo wa watu kuwa na mnepo, watu ambao tayari wanataabika na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
OCHA inasema baa la njaa liliepukwa mwaka jana kutokana na juhudi za kina za jamii, mashirika ya usaidizi wa kibinadamu na mamlaka za nchi husika, pamoja na usaidizi kutoka kwa wahisani.
“Kutokana na misimu mitamu mfululizo bila mvua za kutosha, watu zaidi ya milioni 30 walipatiwa msaada nchini Ethiopia, Kenya na Somalia,” amesema Bi. Msuya.
Hata hivyo amesema dharura bado haijaisha na rasilimali za ziada zinatakiwa kwa dharura ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.
Mashirikia ya kibinadamu yanahitaji jumla ya dola bilioni 7 kwa ajili ya operesheni zake za kiutu na ulinzi kwa wakazi wa Pembe ya Afrika kwa mwaka huu wa 2023.
Mkutano wa leo wa ngazi ya juu uliandaliwa kwa pamoja na Umoja wa Mataifa, Italia, Qatar, Uingereza na Marekani kwa ushirikiano na serikali za Ethiopia, Kenya na Somalia.