Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazao tunapanda sisi, waasi ndio wanavuna- inakwamisha familia - Tsinduka

Philemon Tsinduka (kushoto) na mkewe  Sifa Mwana, wakiwa nyumbani kwao huko Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
UN News/George Musubao
Philemon Tsinduka (kushoto) na mkewe Sifa Mwana, wakiwa nyumbani kwao huko Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Mazao tunapanda sisi, waasi ndio wanavuna- inakwamisha familia - Tsinduka

Masuala ya UM

Hii leo ni siku ya kimataifa ya familia duniani ambapo maudhui ya mwaka huu ni mienendo ya makundi ya watu na familia wakati huu ambapo idadi ya watu inaongeza ingawa kwa kiwango cha chini.

Umoja wa  Mataifa unasema kupungua kwa idadi ya wanafamilia kutoa fursa ya familia kutoa huduma bora zaidi kwa watoto, mathalani elimu na afya.

Lakini ni ndivyo sivyo kwa familia moja huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako pamoja na baba na mama kuhaha kupatia mahitaji familia yao, waasi wanaleta changamoto kwani hata mazao shambani yanavunwa na waasi badala ya kunufaisha familia.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, George Musubao alitembelea Philemon Tsinduka mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini ambapo alimuuliza ni vipi anaweza kuhudumia familia yake ya mke wake pamoja na watoto watatu?

Philemon Tsinduka: Kuishi na mke na watoto na familia nzima unajua hata biblia inasema baba inakupasa uhudumia familia yako. Kuna majukumu mbalimbali ambayo wewe kama mzazi inakupasa kutimizia jamaa lakini inakuwa tatizo. Kuna mahitaji mengi ila kwa ajili ya hali ya nchi unashindwa kuhudumia mahali fulani. Mtoto anaweza kuhitaji kitu kimoja lakini unakosa ila kwa neema ya mwenyezi Mungu tunakuwa tunapata mapato madogo. Lakini kifamilia tupo salama kwani Mungu anaendelea kutuzidishia uzima"

Idhaa ya Kiswahili: Ni matatizo gani anayokumbana nayo katika kuhudumia familia yake.

Philemon Tsinduka: "Kufuatana na ukosefu wa usalama kabisa tunaishi na familia maisha ya kuzorota kwa sababu ya vita maisha yamekwama. Mambao yanakuwa ni shida hata ukiamua kulima shambani nako ni changamoto kwani unakuta waasi wamevamia mashamba yetu na kupora mazao. Watu wakilima mazao na wakikaribia kuvuna, basi waasi wanavamia na kuvuna mazao ya wakazi. Ni kusema maisha yanakuwa magumu kwa sababu ya vita ambayo inaendelea DRC.”

Idhaa ya Kiswahili: Sasa ni namna gani anaweza kuhudumia watoto wake licha ya ukosefu wa usalama?

Philemon Tsinduka: "Si unajua watoto inabidi kuwatunza na kuwalea ili wakue katika mazingira mazuri. Ila kuna mazingira ambamo wanaishi na inasababisha hali yao na namna ya kuwalea inakua numu sana kama vyakula hawapati mlo unaofaa. Tunahaha kutafuta chakula wale washibe kwa faida yamwili, kujua ni jinsi gani ya kupangilia mlo bora na zaidi ya yote kwa sababu mtu anapaswa kula milo mitatu. Hasa utaona inabidi chai ipatikane asubuhi, na mchana halikadhalika.

Ingawa kuna changamoto, Sifa Mwana, mke wa Bwana Tsinduka anaona bado wana furaha kwenye familia yao akisema, " tunaishi na familia vizuri sana tunaamka na kuandaa watoto pamoja. Tunawaandaa ili waende shuleni. Hapa wanakunywa chai na kisha wanabeba maharage kwenda kula shuleni. Tunahangaika kuwahudumia. Tunahakikisha pia wanakuwa wasafi ili kuepuka wasipate magonjwa.

 

Imendaliwa na George Musubao, UNNEWS, Beni, DRC