Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAOC imelaani vikali mauaji ya mwakilishi jumuiya ya Kiislamu Beni DRC 

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akisalimia wakazi wa Beni wakati wa doria huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
UN Photo/Sylvain Liechti
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akisalimia wakazi wa Beni wakati wa doria huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

UNAOC imelaani vikali mauaji ya mwakilishi jumuiya ya Kiislamu Beni DRC 

Amani na Usalama

Mwakilishi wa ngazi ya juu Muungano wa Ustaarabu wa Umoja wa Mataifa (UNAOC), Bwana Miguel Ángel Moratinos, amelaani vikali mauaji ya kinyama ya mwakilishi wa jumuiya ya Kiislamu yaliyofanyika katika mji wa Beni mashariki mwa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wakati wa swala ya jioni katika msikiti wa kati.  

"Sheikh Ali Amin Uthman aliuawa jana Jumamosi wakati watu wenye silaha wasiojulikana walipolivamia msikiti huo na kumpiga risasi."

Mwakilishi huyo wa Muungano wa Ustaarabu wa Umoja wa Mataifa pia amelaani na kushutumu mashambulizi na machafuko ambayo yamekuwa yakifanyika kwa siku za hivi karibuni katika vijiji vya karibu na kukatili maisha ya watu 19.  

Sheikh Uthman mara kwa mara amekuwa akikemea na kulaani msimamo mkali wa vurugu zinazoendelea DRC. 

Mwakilishi huyo wa UNAOC ametoa wito wa "kuheshimu mwezi mtukufu wa wa Ramadhan na anatumai kuwa roho ya huruma, amani na kuheshimiana itatawala."  

Amekumbusha mapendekezo ya mpango wa utekelezaji wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda maeneo ya dini na amesisitiza haki ya kila mtu ya kuabudu na kutekeleza tamaduni za dini zao au imani kwa uhuru na usalama. 

Pia amesema anatumai kuwa wahusika wa uhalifu huo wa kikatili watachukuliwa hatua kali na ametoa pole nyingi kwa familia ya Sheikh Uthman pamoja na familia za waathiriwa wengine waliouawa katika siku chache zilizopita Mashariki mwa DRC.