Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMAS yafanikisha utiaji alama kwenye silaha DRC

Operesheni ya kutia alama kwenye silaha za polisi na jeshi nchini DRC iliendeshwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya hatua dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini, UNMAS na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO.
UN News/George Musubao
Operesheni ya kutia alama kwenye silaha za polisi na jeshi nchini DRC iliendeshwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya hatua dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini, UNMAS na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO.

UNMAS yafanikisha utiaji alama kwenye silaha DRC

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC  ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, kupitia ofisi inayohusika na kutegua mabomu UNMAS, inaendesha kazi ya kuweka alama kwenye silaha za polisi na jeshi la DRC. 

Kazi imefanyika katika mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC, jumla ya silaha 2,500 za jeshi la serikali, FARDC na polisi wa taifa zimetiwa alama na Tume ya Taifa  ya udhibiti wa silaha ndogo ndogo na nyepesi, CNC-ALPC. 

Operesheni hii ilifanikishwa na Umoja wa Mataifa kupitia ofisi yake ya kutegua mabomu, UNMAS kwa lengo la kukabili usambazaji haramu wa silaha jimboni hapa Kivu Kaskazini.  

Tweet URL

Operesheni imefanyika kwa wiki 2 

Herve Kalonda, kutoka CNC-ALPC anasema, “tulifanya opereseni hii ya wiki mbili hapa katika jiji la Beni.  Kwa vyovyote vile tulifanya kila tuwezalo kuweka alama kwenye silaha nyingi iwezekanavyo, lakini kwa hakika bado kuna hitaji kubwa ya silaha nyingi ambazo hazijawekwa alama. Nadhani serikali kwa msaada wa washirika wetu tutaandaa operesheni vingine vya kuweka alama kwenye silaha katika jiji la Beni.  kwa sababu ni muhimu sana kwa usalama wa wakazi.” 

Muteba Kashale Narciss ambaye ni Meya wa jiji la Beni anasema operesheni hii ya kuweka alama kwenye silaha ni muhimu sana katika eneo hili ambamo makundi yenye silaha yanasababisha ukosefu wa usalama.    

Tunataka kufahamu kila silaha nani anamiliki 

Bwana Muteba anasema, “tuna silaha zinazozunguka katika mji huu wa Beni, mji ambamo tuko kwenye operesheni.  Kwa hivyo tukio hili la  kuweka alama kwenye silaha lilikuwa  muhimu kwetu.  Lilikuwa muhimu ili kuwe  na utaratibu, na usalama wa silaha ambazo tunaziona katika jiji.  Hivi kwetu sisi tukio hili  hii lilikuwa muhimu sana na tunasema asante kwa washirika wetu ambao wiko pamoja nasi na ninapozungumzia sisi ni serikali ambayo mimi ndiye mwakilishi wake hapa mjini Beni. Tuna washirika wetu sisi; tuna MONUSCO, UNMAS ambao walitusaidia kwa kampeni hii na iliendelea vizuri katika jiji la Beni.” 

Josia Obat ambaye ni mkuu wa ofisi ya ujumbe wa  Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO mjini Beni amesema, “hatua ilikuwa nzuri ili kila silaha iwe na namba fulani na hii inasaia kila silaha ambayo jeshi inamiliki, inafahamika nani anayo.” 

Silaha 2,500 tu kati ya 10,000 ndio zimewekewa namba 

Bwana Obat amesema iwapo silaha hiyo itafika mikononi mwa waasi au watu wasio na ruhusa ya kutumia silaha hiyo, ikipatikana inaweza kufuatiliwa ili ifahamike imetoka upande gani.“Na hii ni juhudi moja ambayo inaweza kusaidia katika raia ambayo ndio kazi muhimu MONUSCO iko hapa kufanya. Kwa hiyo sisi MONUSCO tumefurahi kuhusika katika kazi hii imefanyika hapa. Wamesema wako na silaha kama 10,000 za kupatia namba, lakini mpaka sasa wameshaweka alama kwenye silaha 2,500. Kwa hiyo bado kazi kubwa kufanyika, na sisi MONUSCO tuko tayari kushirikiana nao ili silaha zote ziwekewe namba na ziwe kwenye mikono ya wale tu wanaopaswa kuzimiliki.” 

Zaidi ya yote, UNMAS imepatia mafunzo timu inayoundwa na wakazi wa eneo la Beni -DRC, ambao wataendelea kufanya kazi ya kuweka alama kwenye silaha.

 

Taarifa hii imeandaliwa na George Musubao wa UN News DRC