Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya changamoto lukuki watu wa Somalia wanaendelea kuonesha mnepo wa hali ya juu:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari wakati akihitimisha ziara yake mjini Moghadishu
UN Photo/Fardosa Hussein
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari wakati akihitimisha ziara yake mjini Moghadishu

Licha ya changamoto lukuki watu wa Somalia wanaendelea kuonesha mnepo wa hali ya juu:Guterres

Amani na Usalama

Katika siku ya pili na ya mwisho ya ziara yake nchini Somalia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewapongeza watu wa Somalia akisema licha ya changamoto lukuki zinazowaandama wameendelea kuwa imara na kuonyesha mnepo wa hali ya juu, akiwataka kuendelea kufanya hivyo kwa ajili ya kizazi hiki na kijacho. 

Antonio Guterres ametoa pongezi hizo katika mkutano na waandishi wa habari wa kuhitimisha zira yake  ya mshikamano mjini Moghadishu akisema tangu alipofika mara ya mwisho nchini humo miaka sita iliyopita kuna mabadiliko kwani sasa Somalia hatua kubwa zimepigwa katika mchakato wa amani, usalama na maendeleo endelevu.

Amempongeza pia Rais wa taifa hilo la Pembe ya Afrika Hassan Sheikh Mohamud kwa juhudi zake za kusongesha mchakato wa amani na usalama na kuainisha umuhimu wa kuwa na ushirikiano imara sio tu na Umoja wa Mataifa bali na nchi wanachama wa serikali ya shirikisho ili kushughulikia tishio la magaidi wa Al-Shabaab.

Katibu Mkuu amewahakikishia Wasomali dhamira ya Umoja wa Mataifa kulisaidia juhudi za taifa hilo na za kikanda katika kulinda haki za binadamu na kupambana na ugaidi na uhalifu wa itikadi kali ikiwemo kupitia mpango wa muungano wa Afrika nchini humo.

Makumi ya maelfu ya watu wamekimbia makazi yao nchini Somalia.
UN Photo/Sourav Sarker
Makumi ya maelfu ya watu wamekimbia makazi yao nchini Somalia.

Baa la njaa bado linanyemelea

Guterres ameongeza kuwa “Ziara yangu ya mwisho mwaka 2017 ilikuwa wakati wa operesheni kubwa ya kuepusha baa la njaa. Leo hii hali kwa mara nyingie ni ya kutia hofu, kwani mabadiliko ya tabianchi yameleta zahma kubwa, misimu 5 isiyo na mvua ambayo si kawaida na ukame tayari umeshakatili Maisha ya watu 43,000 2022 pekee na kutawanya watu wengine milioni 1.4 huku asilimia 80 wakiwa ni wanawake na Watoto.”

Amesem changamoto hizo na ukiongeza na mfumuko wa bei ya chakulaumezifanya jamii za masikini kusukumwa kwenye ukingo wa njaa akikadiria kwamba kati ya sasa na Juni Wasomali milioni 6.5 watakabiliwa na viwango vya juu vya kutokuwa na uhakika wa chakula hali inayodhihirisha kwamba baa la njaa bado linanyemelea.

Amesisitiza kuwa hatua lazima zichukuliwe sasa kuepusha janga kubwa Zaidi hasa akiwasihi wahisani kunyoosha mkono Zaidi kwani ombi la kibinadamu kwa ajili ya Somalia 2023 ambalo n idola bilioni 2.6 zimefadhiliwa kwa asilimia 15 pekee hadi sasa.
Hata hivyo Katibu Mkuu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani amewapa matumaini Wasomali kwa ahadi ya Umoja wa Mataifa kushikamana nao katika kusongesha amani na usalama, maendeleo endelevu, haki za binadamu na ujenzi wa mustakbali bora kwa Wasomali wote.