Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa watoa dola milioni 250 kufadhili shughuli za dharura

Sadio Yalcouyé mtaalamu wa lishe, akitayarisha maziwa ya F-100 na F - 75 kwa watoto wenye utapiamlo (MAS) waliolazwa hospitalini katika Kitengo cha Urejesho na Elimu ya Lishe Bora (URENI) cha hospitali ya Ménaka, Mali.
© UNICEF/N’Daou

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametangaza kutenga dola milioni 250 kutoka Mfumo mkuu wa dharura CERF ili kukabiliana na njaa na kushughulikia dharura zisizo na ufadhili wa kutosha.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa tangazo hilo mbele ya waandishi wa habari jijini Addis Ababa nchini Ethiopia ambapo ameenda kuhudhuria kikao cha 36 cha kawaida cha mkutano wa ngazi ya juu ya viongozi wa Muungano wa Afrika, AU jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Guterres amewaambia waandishi wa habari kuwa huo ni mgao mkubwa zaidi kuwahi kutokea wa CERF, na unakuja kutokana na ongezeko la asilimia 25 la idadi ya watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu a,bao ni takribani milioni 339.

Kati ya nchi 18 zitakazofikiwa na msaada huo nchi 12 zipo barani Afrika.

Rasilimali zitakazopatikana kutokana na fedha hizo zinatarajia kuwasaidia baadhi ya watu walio hatarini zaidi katika baadhi ya maeneo yenye migogoro iliyosahaulika duniani kote.