Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yazindua mpango wa kuondoa pengo la tiba ya saratani ya titi

Kipimo cha mara kwa mara cha saratani ya titi kinaweza kuepusha kushamiri kwa ugonjwa huo.
© Unsplash/National Cancer Institute
Kipimo cha mara kwa mara cha saratani ya titi kinaweza kuepusha kushamiri kwa ugonjwa huo.

WHO yazindua mpango wa kuondoa pengo la tiba ya saratani ya titi

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO hii leo limezindua mpango wa kutokomeza saratani ya titi duniani, ikilenga kuokoa maisha ya watu milioni 2.5 ifikapo mwaka 2040 kwa kuondoa pengo la upatikanaji wa tiba kati ya nchi za kipato cha juu na zile za kipato cha chini na kati.

Uzinduzi huo umefanyika ikiwa ni siku moja kabla ya maadhimisho ya siku ya saratani  duniani, tarehe 4 mwezi Februari.

WHO inasema kila mwaka, zaidi ya wanawake milioni 2.3 wanabainika kuwa na saratani ya titi, na kufanya saratani hiyo kuwa ni saratani inayoongoza kwa kuathiri watu wazima duniani.

Kuugua saratani ya titi nchi maskini ni sawa na hati ya kifo

Ijapokuwa idadi ndogo ya nchi zenye kipato cha juu zimeweza kupunguza vifo vitokanavyo na saratani hiyo kwa asilimia 40 tangu mwaka 1999, kwa wanawake walio nchi  maskini, moja ya changamoto kubwa ni kupata vipimo vya ugonjwa huo kwa wakati.

“Uwezakano wa mtu kupona saratani kwa nchi za kipato cha chini na kati ni kati ya asilimia 50 au chini yah apo,” amesema Dkt. Bente Mikkelsen akizungumza na waandishi wa habari jijini Geveva, USwisi hii lee.

Hata hivyo kwa nchi za kipato cha juu, uwezekano wa mtu kupona saratani ya titi ni zaidi ya asilimia 90 kwa kuwa wana uwezo wa kupata tiba bora.

Manusura wa saratani  ya titi nchini Jamaica
WHO
Manusura wa saratani ya titi nchini Jamaica

Mkakati wa kuondoa pengo la usawa kwenye tiba

Ili kuondoa pengo hilo la usawa, WHO imezindua Mkakati dhidi ya Saratani ya Titi wenye lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa asilimia 2.5 kila mwaka.

“Nchi zenye mifumo dhoofu ya afya zina uwezo mdogo wa kudhibiti mzigo wa saratani ya titi. Inaweza shinikizo kubwa kwa mtu mmoja mmoja, familia, jamii, mifumo ya afya na uchumi, hivyo ni lazima iwe kipaumbele cha kwanza kwa wizara za afya na serikali kila mahali,” ameesma Dkt. Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

Amekumbusha kuwa mbinu na utaalamu wa kuzuia saratani ya titi upo, halikadhalika mbinu za kuokoa maisha na kwamba “WHO inasaidia zaidi ya nchi 70 hasa zenye vipato vya chini na kati kuchunguza mapema saratani kwa haraka, kutibu na kumpatia kila mtu matumaini ya kutokuwa na saratani siku za usoni.”

Mpango unafanya nini?

Ili kutoa usaidizi kwa mujibu wa mahitaji mahsusi ya nchi na kutoa mwongozo, mpanog huo una misingi mitatu: Uendelezaji wa mbinu za kudhibiti afya na kubaini ugonjwa; uchunguzi kwa wakati na tiba kwa kutumia dawa fanisi.

Ifikapo mwaka 2040, zaidi ya wagonjwa milioni 3 na vifo milioni moja vinatarajiwa kuweko kila mwaka duniani kote huku asilimia 75 ya vifo hivyo vikitarajiwa kutokea nchi za vipato vya chini na kati.

Kwa kweli hatuwezi kuepuka saratani ya titi iwapo tunataka kutatua changamoto ya saratani kwenye hizi nchi,” amesema Dkt. Ben Anderson, Afisa wa Tiba katika mpango wa kimataifa wa Saratani  ya Titi wa WHO.

“WHO inasema saratani hiyo imejikita zaidi miongoni mwa wanaume na wanawake, na inawezekana ndio sababu ya wanawake kufa kwa saratani duniani.

Saratani  ya titi ni  ya kwanza au ya pili katika sababu za vifo vitokanavyo na saratani kwenye asilimia 95 ya nchi, “kwa hiyo kuwa na mpango huu kutajenga msingi wa kusongesha mazingira bora ya kuondokana na ugonjwa huo siku za usoni.”