Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu bilioni tano hawajalindwa kutokana na viambato vinavyosababisha ugonjwa wa moyo

Watu bilioni tano hawajalindwa kutokana na viambata vinavyosababisha ugonjwa wa moyo
© WHO/Sergey Volkov
Watu bilioni tano hawajalindwa kutokana na viambata vinavyosababisha ugonjwa wa moyo

Watu bilioni tano hawajalindwa kutokana na viambato vinavyosababisha ugonjwa wa moyo

Afya

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa leo Jumatatu Januari 23, 2023 imebainisha kuwa watu bilioni tano duniani hawajalindwa dhidi ya viambato hatari vya mafuta vilivyoko katika bidhaa za vyakula vinazozalishwa viwandani na hivyo kuongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo na kifo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO linasema tangu mwaka 2018 lilipotoa wito wa kuondolewa kimataifa kwa viambato vya mafuta vinavyozalishwa viwandani, ufikiaji wa watu wa sera za matumizi bora umeongezeka karibu mara sita na kwamba nchi 43 sasa zimetekeleza sera za hatua bora kukabiliana na mafuta katika chakula, huku watu bilioni 2.8 wakiwa wamelindwa duniani kote.

Hata hivyo utafiti wa WHO umebaini kuwa hatua hii iliyofikiwa bado inaacha hatarini watu bilioni 5 duniani kote kutokana na athari mbaya za afya za viambato vya mafuta vinavyozalishwa viwandani na lengo la kimataifa la kutokomeza kabisa viambato hivyo hatari katika vyakula kufikia mwaka huu wa 2023 likisalia kuwa haliwezi kufikiwa kwa wakati huu, unaeleza utafiti wa WHO.

WHO inabainisha kuwa viambato vya mafuta vilivyozalishwa viwandani (pia huitwa asidi ya mafuta yanayozalishwa viwandani) hupatikana kwa wingi katika vyakula vilivyofungashwa mathalani kwenye makopo au mifuko, bidhaa zilizookwa na mafuta ya kupikia. Viambato hivyo huwekwa, pamoja na sababu nyingine ili bidhaa hizo ziwe na ladha nzuri na kudumu kwa muda mrefu. WHO inathibitisha kuwa ulaji wa viambato vya mafuta kila mwaka kote duniani husababisha hadi vifo 500,000 vya mapema kutokana na ugonjwa wa moyo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesisitiza akisema, "viambato vya mafuta havina faida yoyote inayojulikana, na ni hatari kubwa za kiafya ambazo huleta gharama kubwa kwa mifumo ya afya. Kinyume chake, kuondoa viambato vya mafuta katika bidhaa kuna gharama nafuu na kuna faida kubwa kwa afya. Kwa urahisi, viambato vya mafuta katika vyakula ni kemikali yenye sumu ambayo inaua, na haipaswi kuwa na nafasi katika chakula. Ni wakati wa kuiondoa mara moja na kwa wote."

Ripoti hiyo, inayoitwa "Hesabu kuelekea mwaka 2023 - Ripoti ya WHO kuhusu uondoaji wa viambato vya mafuta duniani 2022", ni ripoti ya kila mwaka ya hali ilivyo iliyochapishwa na WHO kwa ushirikiano na shirika la Resolve to Save Lives, kufuatilia maendeleo kuelekea lengo la kuondoa viambato vya mafuta katika bidhaa za viwandani kufikia mwaka huu wa 2023.