Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi wa mauaji ya watu 28 huko Burkina Faso uwe huru na ufanyike haraka: UN

Mwanajeshi kutoka Burkina Faso akiwa katika ulinzi kwenye mpaka baina ya Burkina Faso, Mali na Niger wakati wa operesheni ya kijeshi dhidi ya washukiwa wa ugaidi.
© Michele Cattani
Mwanajeshi kutoka Burkina Faso akiwa katika ulinzi kwenye mpaka baina ya Burkina Faso, Mali na Niger wakati wa operesheni ya kijeshi dhidi ya washukiwa wa ugaidi.

Uchunguzi wa mauaji ya watu 28 huko Burkina Faso uwe huru na ufanyike haraka: UN

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Türk hii leo ametaka uchunguzi wa mauaji ya watu 28 huko kaskazini-magharibi mwa Burkina Faso uwe huru na bila kuegemea upande wowote.

Kamishna Mkuu Türk amesema hayo kupitia taarifa iliyotolewa Ijumaa na ofisi yake mjini Geneva Uswisi kufuatia mauaji hayo ya tarehe 30 na 31 mwezi Desemba mwaka jana na kisha miili yao kubainika kwenye mji wa Nouna, jimbo la Kossi ukanda wa Boucle du Mouhoun nchini Burkina Faso.

Mauaji yanatokana na kulipiza kisasi

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ofisi ya Kamishna wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Burkina Faso inalaumu kikundi cha wanamgambo cha VDP au Volontaires pour la Defense de la Patrie kwa mauaji hayo ikisema, “wafuasi wa kikundi hicho walivamia mji huko na kuua wanaume 28 ikiwa ni kulipiza kisasi kwa shambulio la awali dhidi ya kituo cha kikundi hicho usiku uliotangulia.”

Kikundi hicho cha VDP kinadai kuwa shambulio dhidi ya kituo chake liliendeshwa na wafuasi wa kikunsi cha waasi cha Al-Qaeda chenye uhusiano na Jama’at Nasr al Islam wal Muslimin au JNIM.

“Inatia hamasa ya kwamba mamlaka za mpito Burkina Faso zimetangza kuchunguza tukio hilo. Natoa wito kwa mamlaka hizo zihakikishe uchunguzi unafanyika haraka, kwa kina, bila upendeleo wowote na uwe wa uwazi ili hatimaye wahusika wawajibishwe bila kujali nafasi au vyeo vyao,” amesema Bwana Türk .

Wakimbizi wa ndani wakisubiri mgao wa chakula kwenye kituo cha Gorom-Gorom nchini Burkina Faso
© WFP/Cheick Omar Bandaogo
Wakimbizi wa ndani wakisubiri mgao wa chakula kwenye kituo cha Gorom-Gorom nchini Burkina Faso

Ameongeza kuwa tayari ametuma barua kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso akisisitiza ujumbe huo na zaidi ya yote waathirika na wapendwa wao hawatarajii kingine chochote zaidi ya hatua hizo.

Tarehe 2 mwezi huu wa Januari, msemaji wa serikali ya mpito ya Burkina Faso alisema uchunguzi umeanza na serikali inapinga aina yoyote ile ya unyanyasaji au ukiukaji wa haki za binadamu kwa misingi yoyote ile na kusisitiza azma ya mamlaka hizo kulinda raia wote bila ubaguzi wowote.

Hofu ya OHCHR kuhusu ukiukaji wa haki kwenye ajira

Katika siku zilizopita Kamishna Mkuu Türk alionesha wasiwasi wake kwa mamlaka za Burkina Faso kuhusu hatari ya uwezekano wa ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye utumikishaji, upatiaji silaha na upelekaji wa wanamgambo kwenye maeneo mbalimbali nchini humo.

“Kuna udharura wa kuimarisha kanuni za uchunguzi wa watu kabla ya ajira, mafunzo kuhusu haki za binadamu kabla ya usambazaji wa vikosi vya kijeshi, usimamizi wa vikosi hivyo kutoka kwa majeshi ya usalama na kuhakikisha ujumuishi na uwazi wakati wa ajira,” alisema Bwana Türk.

Tangu mwaka 2015 Burkina Faso imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la mashambulizi kutoka vikundi vyenye misimamo mikali ya kidini vyenye uhusiano na Al-Qaeda na ISIS au Daesh, mashambulizi ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine milioni mbili kufurushwa makwao