Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaondoa kipengele cha kutaka wanaouzia silaha DRC kutoa taarifa mapema

Walinda amani wakifanya doria huko Butembo, Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kuhakikisha usalama wa jamii.
UN Photo/Martine Perret
Walinda amani wakifanya doria huko Butembo, Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kuhakikisha usalama wa jamii.

UN yaondoa kipengele cha kutaka wanaouzia silaha DRC kutoa taarifa mapema

Amani na Usalama

Hatimaye hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotengua kipengele cha azimio lake la awali namba 1533 linalotaka nchi zinazouzia silaha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kutoa kwanza taarifa kwa kamati ya Baraza hilo inayohusika na vikwazo dhidi ya taifa hilo la Maziwa Makuu barani Afrika. 

Azimio la leo na yaliyotangulia yanasema nini 

Azimio hilo namba 2667 lililopitishwa leo kwa kauli moja na wajumbe wa Baraza hilo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, linasema uamuzi wa leo ni kwa mujibu wa sura ya VII ya Chata ya Umoja wa Mataifa na kwamba, “masharti ya kutoa taarifa yaliyowekwa kwenye aya ya 5 ya azimio namba 1807 la mwaka 2008 hayatatumika tena.” 

 Aya hiyo ya 5 ya azimio namba 1807 la mwaka 2008 ilisema, “nchi zote zinapaswa kutoa taarifa kwanza kwa Kamati kuhusu usafirishaji wa silaha au vifaa vyovyote vinavyohusiana kwenda DRC au msaada wowote ule, ushauri, mafunzo yanayohusiana n ajeshi nchini DRC isipokuwa vilivyoelezwa kwenye aya ndogo (a) na (b) ya aya kubwa ya 3 na kusisitiza umuhimu wa taarifa hiyo iwe na taarifa za msingi kama itakavyofaa mfano mtumiaji, tarehe ya shehena kufika na ratiba  ya safari.” 

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu MONUSCO nchini DRC wakitoa msaada wa kibinadamu kwa wakazi Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini kufuatia machafuko mashariki mwa nchi hiyo.
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu MONUSCO nchini DRC wakitoa msaada wa kibinadamu kwa wakazi Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini kufuatia machafuko mashariki mwa nchi hiyo.

Sharti kutoka kwa wajumbe wa Baraza kwenda kwa DRC 

Hata hivyo azimio la leo linasema pamoja na kutolewa kwa kipengele hicho cha utoaji wa taarifa, “serikali ya DRC inatakiwa kuwasilisha ripoti ya siri kwa Baraza la Usalama kabla ya tarehe 31 mwezi Mei mwaka 2023 inayoelezea kwa kina juhudi zake za kuhakikisha  usalama na usimamizi fanisi, uhifadhi, uwekaji alama, ufuatiliaji, usalama wa bohari za silaha pamoja na juhudi za kukabili usafirishaji haramu wa silaha na matumizi kule ambako hayatakiwi.” 

Azimio hilo pia limesisitiza kuwa hatua zilizowekwa kwenye aya ya 1 ya azimio 1807 la mwaka 2008 yanaendelea kuzingatiwa kwa vyombo visivyo vya kiserikali na watu wanaoendesha shughuli zao DRC. 

Aya hiyo ilikuwa inaonya nchi zote kuhakikisha kuwa zinazuia upelekaji, usambazaji wa moja kwa moja au kwa njia nyingine kutoka maeneo yao au kutekelezwa na wananchi wao kupitia vyombo vya usafiri vyenye bendera za nchi hizo silaha au vifaa vyovyote vile vya kijeshi au msaada wa fedha kwa makundi yaliyojihami au watu binafsi nchini DRC. 

Azimio 2667 linaondoa jukumu la ufuatiliaji wa vikwazo dhidi ya DRC kutoka MONUSCO na badala yake sasa jukumu linasalia kuwa la Kamati ya Vikwazo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wapiganaji wa M23 wakielekea Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
MONUSCO/Sylvain Liechti
Wapiganaji wa M23 wakielekea Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

Muda wa MONUSCO waongezwa hadi Desemba 2023 

Mapema wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo kwa kauli moja wamepitisha azimio la kuongeza kwa mwaka mmoja zaidi hadi tarehe 20 mwezi Desemba mwaka 2023, muda wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MONUSCO uliokuwa umalizike leo tarehe 20 mwezi Desemba. 

Baadhi ya wajumbe waliochangia baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, wakiwemo wawakilishi wa kudumu wa Kenya, Ghana na Falme za kiarabu, wamesema “kuongezwa muda kwa MONUSCO kutasaidia kuimarisha amani mashariki mwa DRC ambako kwa sasa kuna changamoto kubwa ya amani.” 

Ufaransa ndio iliandaa maazimio haya

Mapema akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kupitishwa kwa azimio hilo namba 2666, Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa Nathalie Estival-Broadhurst ambao ndio waliandaa rasimu yake, amesema “Azimio linapatia MONUSCO mamlaka bora zaidi ya kulinda raia, kusaidia mpango wa kuvunja makundi ya waasi na kuwajumuisha kwenye jamii na pia marekebisho ya  ulinzi DRC. “

Halikadhalika, kwa mujibu wa Balozi Estival-Broadhurst, azimio linapatia MONUSCO uwezo wa kutoa usaidizi wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini humo mwezi Desemba mwaka 2023.

Fabien Mwingwa akiwa ofisi kwake. Yeye ni mpiganaji wa zamani wa msituni na sasa ameajiriwa na MONUSCO, Goma jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC kama askari wa zimamoto.
UN/ Eskinder Debebe
Fabien Mwingwa akiwa ofisi kwake. Yeye ni mpiganaji wa zamani wa msituni na sasa ameajiriwa na MONUSCO, Goma jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC kama askari wa zimamoto.

“MONUSCO itaendelea pia kufuatilia hali ya haki za binadamu, kusaidia mfumo wa sheria na kupambana na ukwepaji sheria,” amesema Mwakilishi huyo wa kudumu wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa.

Azimio pia limeruhusu MONUSCO isaidie mchakato wa Nairobi na Luanda kuhusu amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na vile vile kushirikiana na jeshi la DRC, FARDC na lile la kikanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.