Usimamizi mzuri wa uhamiaji utaleta ustawi kwa kila mtu duniani- Guterres
Usimamizi mzuri wa uhamiaji utaleta ustawi kwa kila mtu duniani- Guterres
Ikiwa leo ni siku ya uhamiaji duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameangazia umuhimu wa haraka wa kuweko kwa usimamizi mzuri wa uhamiaji salama unaojikita kwenye mshikamano, ubia na kuheshimu haki za binadamu.
Katika ujumbe wake wa siku hii yenye maudhui Chukua Hatua, Guterres amesema usimamizi mzuri wa uhamiaji ni muhimu kwa kutambua ukweli kwamba uhamiaji ni sehemu ya maisha na huchochea hali bora kwani “huendeleza kubadilishana kwa maarifa na mawazo, na huchangia kwenye ukuaji wa uchumi. Huwezesha mamilioni ya watu kufuata furs ana kuboresha maisha yao.”
Uhamiaji usiosimamiwa hutumbukiza watu kwenye hatari
Hata hivyo Katibu Mkuu amesema usimamizi mbaya wa uhamiaji ni chanzo cha machungu makubwa. Hutumbukiza watu kwenye dimbwi la wasafrishaji haramu, ambako wanakabiliwa na utumikishwaji , manyanyaso na hata kifo.
Amesema miaka mitano iliyopita, Umoja wa Mataifa ulipitisha Mkataba wa Kimataifa kwa ajili ya Uhamiaj Usalama, wenye Mpango na Kanuni.
“Huu umekuwa nyaraka muhimu ya kuzingatia na sehemu ya nchi wanachama kutumia kutathmini vitendo vyao, kuimarisha ushirikiano na kupanua fursa za njia za uhamiaji,” amesema Katibu Mkuu.
Ingawa hivo amesema mikakati hiyo badala ya kuwa maadili ya kuzingatiwa imesalia kuwa hatua zinazozingatiwa kwa kuchagua.
“Leo hii na kila siku, lazima tufanye kazi kuelekea uhamiaji salama, wenye mpango na maslahi kwa wote,” amesema Katibu Mkuu akisema uhamiaji huo uwe na maslani pia kwa jamii wanakotoka, kwenye eneo la mpito na eneo wanalokwenda wahamiaji.
Amesema ni kwa pamoja tunaweza kupata mustakabali salama na wenye ustawi kwa wote.
Uhamiaji una umri sawa na uwepo wa binadamu duniani
Amy Pope, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM, amesema uhamiaji umekuweko duniani tangu kuweko kwa binadamu.
“Hata hivyo hivi sasa uhamiaji umekuwa mgumu kuanzia pwani ya Djibouti hadi eneo la Darien huko Amerika ya Kusini,” amesema Bi. Pope.
Zaidi ya hayo, idadi ya watu wanaohama makwao inazidi kuongezeka kila uchao kutokana na mapigano, kukimbia mateso, mabadiliko ya tabianchi na tofauti za kiuchumi, huku wakiwa na fursa ndogo ya kuchagua wapi pa kwenda kwa ajili ya usalama na kujipatia kipato.
Mkuu huyo wa IOM anasema huu ni wakati muhimu sana kwa watu walio njiani kusaka usalama, kwa wale watakaotaka kuhama siku za usoni na kwa wale wanaotaka kusalia waliko.
“Tunapaswa kuja pamoja na majawabu yanayopatia kipaumbele watu na yanayotokana na ushahidi kwa watu wanaotaka kubakia kwenye jamii zao na kwa wale wanaolazimika kuhama. IOM tumejikita kwa kwenye kutatua changamoto hizi kwa sababu tunatambua uhamiaji ukisimamiwa vema ni msingi wa maendeleo endelevu, ustawi na maendeleo,” amesema Bi. Pope.
Tazama ujumbe mzimwa Mkuu huyo wa IOM hapa.
Siku ya uhamiaji duniani ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 4 Desemba mwaka 2000 kwa azimio namba A/RES/55/93 kwa kutambua ongezeko la wahamiaji duniani.