Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Meli iliyobeba msaada wa chakula kwa ajili ya wananchi wa Ethiopia yatia nanga Djibout

WFP ikipakia shehena ya ngano kwenye meli
© WFP/Anastasiia Honcharuk
WFP ikipakia shehena ya ngano kwenye meli

Meli iliyobeba msaada wa chakula kwa ajili ya wananchi wa Ethiopia yatia nanga Djibout

Msaada wa Kibinadamu

Hatimaye meli iliyokodiwa na Umoja wa Mataifa iliyokuwa imepakia tani 23,000 za ngano kutoka Ukraine inayopeleka kwa mamilioni ya watu wenye uhitaji wa chakula nchini Ethiopia ilitia nanga katika nchi jirani ya Djibouti.

Ukame mkali kwa zaidi ya misimu minne mfululizo umewaacha watu milioni 22 kutoka nchi za pembe ya Afrika ambazo ni Ethiopia, Kenya na Somalia katika uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu.  Vita ya Ukraine na Urusi ilifanya hali kuwa mbaya zaidi kwa mataifa haya kwakuwa wanategemea nafaka kutoka Ukraine kwa ajili ya msaada wa chakula.

Lakini sasa Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP kanda ya Afrika Mashariki Mike Dunford anasema meli yenye shehena ya tani 23,000 za ngano imetia nanga katika bandari ya nchi jirani ya Djibouti tayari kusafirishwa kuingia Ethiopia.

Dunford anasema “Chakula kilicholetwa na meli hii ya kamanda shujaa kitalisha watu milioni 1.5 kwa mwezi mmoja nchini Ethiopia. Hii italeta utofauti mkubwa sana kwa watu ambao kwa sasa hawana chochote. Na sasa WFP itaweza kuwapatia mahitaji yao ya kimsingi.”

Watu wanasubiri msaada wa chakula huko Tigray, Ethiopia
© UNOCHA/Mulu Tesfay Araya
Watu wanasubiri msaada wa chakula huko Tigray, Ethiopia

Tangu Umoja wa Mataifa kufanikisha kusainiwa makubaliano ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi ulioruhusu meli ya Ukraine kusafirisha nafaka, tayari meli takriban 114 zilizobeba shehena ya tani milioni 1.2 za chakula zimesafirishwa katika soko la kimataifa na maeneo ya misaada kama hii ilitoleta nafaka Ethiopia na Mkuu huyo wa Kanda wa WFP anasema "Tayari tumeona bei ya ngano imepungua kwa asilimia 15 duniani kote tangu mpango wa Bahari Nyeusi kuanza. Tunachotaka kuona ni chakula kinatiririka zaidi.

Tunahitaji, kwa mtazamo wa WFP, mamilioni ya tani katika eneo hili. Nchini Ethiopia pekee, robo tatu ya kila kitu tulichokuwa tukisambaza kilitoka Ukraine na Urusi.”


TAGS: Ukraine, WFP,Ethiopia, Djibouti, Somalia, Kenya,Msaada wa kibinadamu, Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi