Silaha nimesalimisha sasa natengeneza simu na maisha ni bora sana- kijana DRC
Silaha nimesalimisha sasa natengeneza simu na maisha ni bora sana- kijana DRC
Katikati ya mji wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kuna vioski lukuki vya kutengeneza simu janja na miongoni mwao ni cha vijana wawili wanufaika wa mradi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, mradi wa kupunguza ghasia, CVR katika taifa hilo lililoghubikwa na ghasia mashariki mwa nchi.
Kibandani ni vijana wawili, Promesse Musole na Gedeon Ishara, miongoi mwa vijana 40 wanufaika wa mradi huo uliowawezesha kupata mafunzo ya miezi sita (6) ya kutengeneza simu janja.
Akiwa kwenye kioski hicho Promesse anasema “nilipata mafunzo ya kutengeneza simu, na sasa kupitia mafunzo Niko hapa. Kabla ya mafunzo maisha yalikuwa mabaya sana. Lakini kwa leo nashukuru Mungu naweza kupata fedha kidogo kulinda familia.”
Promesse akionekana makini kutengeneza simu akaulizwa kuhusu alichopitia vitani, “ndio wakati tulikuwa tunapitia hayo na tukaweza kutoka na tukapata mafunzo ya kutengeneza simu na hayo yote ya zamani tulishaacha.”
Yaliyopita yamepita, sitorudi tena msituni- Promesse
Hakutaka kufunguka zaidi kwa kuwa wahenga wanasema, ‘yaliyopita si ndwele tugange yajayo’ na akatoa ujumbe kwa wale ambao bado wako msituni.
“Wale vijana wengine kupitia mafundisho tuliyopata ni bora waondoke waje wajiunge nasi. Hakuna jambo lolote ni kupoteza wakati na wanaweza kupoteza maisha. Waje waungane nasi maisha yanaweza kuendelea vizuri na wao wanaweza kuona kuwa kule waliko hakuna maana yoyote. Wakija hapa tutawaelekeza vizuri kwa kuwa hata sisi hatutaki hata kurudi tena.”
Promesse akawa na ujumbe kwa wale wanaolaghai vijana waende msituni akisema wanapoteza wakati wao bure, “waje wafanye kazi za mikono, wana mikono na wana nguvu. tutumike kuendeleza mbele nchi yetu, na tuendeleza usalama.”
Bila MONUSCO na UN mimi nisingalikuwa hapa
Kwa MONUSCO, Promesse akatoa shukrani kubwa akisema bila ujumbe huo asingalikuwa hapa aliko sasa. “MONUSCO ilifanya vizuri sana kwa kuweza kutupatia huu mradi. Kama si wao nisingalikuwa mimi nilivyo sasa.”
Promesse amesema na Umoja wa Mataifa nao umemtoa mbali anatoa shukrani lakini kwa serikali ya DRC, “tafutieni vijana kazi ambazo wanaweza kufanya. Vijana wanaenda porini kushika silaha kwa sababu wanakosa kazi halali ya kufanya ndio maana wanakwenda porini.”
Ombi la Promesse ni mtaji zaidi ili waweze kununua vifaa vingi zaidi na vya kisasa, “ikiwezekana watupatie mtaji ili kioski chetu kiweze kupanuka na maisha yetu yasonge mbele.”
Nataka kuwa mchuuzi mkubwa niende kununua bidhaa Dubai- Gedeon
Kwa Gedeon, yeye hakutumikishwa vitani lakini alikuwa mtaani hana chochote cha kufanya na hivyo kuwa hatarini kutumbukizwa kwenye ghasia.
“Maisha yalikuwa magumu sana, huna pa kutafutia. Lakini sasa napata fedha kidogo, naweza kununua nguo,” anasema Gedeon.
Akiongea kwa Bashasha anasema shukrani kubwa ni MONUSCO na tayari ameweza kumiliki nyumba na ameoa.
“Vijana wanaozagaa mtaani waje tufanye kazi pamoja kama wana moyo wa kufanya kazi. Kwa Umoja wa Mataifa nawashukuru kwani bila wao nisingalikuwa hapa,” amesema Gedeon.
Na matarajio yake ni kuwa mfanyabiashara mkubwa aende nje ya nchi kuleta vifaa vya kisasa.
Mradi wa MONUSCO CVR
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, miradi ya CVR ilianzishwa na MONUSCO mwaka 2017 ikilenga kusaidia kusongesha amani kupitia miradi kama vile kupatia jamii mbinu za kujipatia kipato, ujenzi wa miundombinu, stadi za kiufundi, kuzuia ukatili wa kijinsia, ulinzi wa watoto, waliotumikisha vitani na vijana walio hatarini.