Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo dhidi ya UKIMWI yakidorora, mamilioni ya watu hatarini 

Mandisa Dukashe na familia yake ni wakazi wa Eastern Cape, Afrika Kusini. Mandisa ni muuguzi na anahusika na udhibiti wa VVU na yeye mwenyewe anaishi na VVU. Lakini mumewe na binti zake wamepima VVU na hawana virusi hivyo.
AFP PHOTO/MUJAHID SAFODIEN
Mandisa Dukashe na familia yake ni wakazi wa Eastern Cape, Afrika Kusini. Mandisa ni muuguzi na anahusika na udhibiti wa VVU na yeye mwenyewe anaishi na VVU. Lakini mumewe na binti zake wamepima VVU na hawana virusi hivyo.

Maendeleo dhidi ya UKIMWI yakidorora, mamilioni ya watu hatarini 

Afya

Maendeleo katika kuzuia Virusi Vya UKIMWI, VVU, na matibabu vinadorora kote ulimwenguni, na kuwaweka mamilioni ya watu katika hatari kubwa. Imeeleza ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI, UNAIDS. 

Takwimu mpya kutoka kwa UNAIDS kuhusu mapambano dhidi ya VVU duniani zinaonesha kwamba katika miaka miwili iliyopita ya coronavirus">COVID-19 na majanga mengine ya kimataifa, maendeleo dhidi ya janga la VVU yamedorora, rasilimali zimepungua, na matokeo yake mamilioni ya maisha yako hatarini.  

Ripoti hiyo mpya kwa jina ‘In Danger’ yaani ‘Hatarini’, imezinduliwa kabla ya Kongamano la Kimataifa la UKIMWI huko Montreal, Canada. 

Ulimwenguni idadi ya maambukizi mapya ilipungua kwa asilimia 3.6 pekee kati ya mwaka 2020 na mwaka 2021, ukiwa ni upunguaji mdogo wa kila mwaka kwa maambukizi mapya ya VVU tangu 2016. Ulaya Mashariki na Asia ya kati, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, na Amerika ya Kusini zote zimeshuhudia ongezeko la maambukizi ya VVU ya kila mwaka kwa miaka kadhaa. Katika Asia na Pasifiki, eneo lenye watu wengi zaidi duniani, takwimu za UNAIDS zinaonesha maambukizi mapya ya VVU yanaongezeka kwa mwaka kwa miaka kadhaa. Maambukizi ya kupanda katika mikoa hii ni ya kutisha. Katika Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika maendeleo ya haraka kutoka miaka ya nyuma yalipungua kwa kiasi kikubwa mwaka 2021. Kuna baadhi ya taarifa chanya, na kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU katika Afrika Magharibi na Kati na katika Karibea, lakini hata katika maeneo haya, mapambano dhidi ya VVU yanatishiwa na uhaba wa rasilimali. 

Winnie Byanyima ambaye ni mkurugenzi mtendaji mpya wa UNAIDS akiwa kwenye moja ya mikutano ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kwenye Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Amanda Voisard
Winnie Byanyima ambaye ni mkurugenzi mtendaji mpya wa UNAIDS akiwa kwenye moja ya mikutano ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kwenye Umoja wa Mataifa.

"Takwimu hizi zinaonesha mapambano dhidi ya UKIMWI duniani katika hatari kubwa. Ikiwa hatufanyi maendeleo ya haraka basi tunapoteza, kwani janga hili linastawi katikati ya COVID-19, kufurushwa kwa watu wengi, na majanga mengine. Hebu tukumbuke mamilioni ya vifo vinavyoweza kuzuilika tunavyojaribu kukomesha.” Amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Winnie Byanyima. 

Kudorora kwa maendeleo kulimaanisha takriban maambukizi mapya milioni 1.5 yalitokea mwaka jana, yaaani zaidi ya watu milioni 1 zaidi ya malengo ya kimataifa. 

Ukosefu wa usawa uliobainishwa ndani na kati ya nchi, unakwamisha maendeleo katika mapambano dhidi ya VVU, na VVU inapanua zaidi ukosefu huo wa usawa. 

Maambukizi mapya yalitokea miongoni mwa wanawake wachanga na wasichana balehe, na maambukizi mapya kila baada ya dakika mbili katika watu hawa mwaka wa 2021. Athari za VVU kijinsia, hasa kwa vijana wa kike na wasichana wa Kiafrika, zilitokea katikati ya kukatizwa kwa huduma muhimu za matibabu na kinga ya VVU, mamilioni ya wasichana walioacha shule kwa sababu ya magonjwa ya milipuko, na kuongezeka kwa mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia. Katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, wasichana na wanawake vijana wana uwezekano mara 3 wa kupata VVU kuliko wavulana na wanaume vijana. 

Wakati wa usumbufu wa miaka michache iliyopita, idadi kubwa ya watu wameathiriwa katika jamii nyingi na kuongezeka kwa maambukizi katika maeneo mengi. Kwa mfano, huko El Salvador kati ya mwaka 2019 na 2021 maambukizi ya VVU kati ya wanaume wanaofanya ngono na wanaume yalikaribia mara mbili, na kuongezeka mara 8 kati ya watu waliobadili jinsia. Takwimu za UNAIDS zilionesha maendeleo duni katika kuondoa sheria za adhabu zinazoongeza hatari ya kuambukizwa VVU na vifo kwa watu waliotengwa ikiwa ni pamoja na watu wa LGBTI, watu wanaojidunga dawa za kulevya na wafanyabiashara ya ngono. 

Kukosekana kwa usawa wa rangi pia kunaongeza hatari za VVU. Nchini Uingereza na Marekani, kupungua kwa ugunduzi mpya wa VVU kumekuwa kukubwa miongoni mwa watu Weupe kuliko watu Weusi. Katika nchi kama vile Australia, Canada na Marekani, viwango vya kupata VVU ni vya juu zaidi katika jumuiya za kiasili kuliko katika jumuiya zisizo za kiasili. 

Ripoti hiyo pia inaonesha kwamba juhudi za kuhakikisha kwamba watu wote wanaoishi na VVU wanapata matibabu ya kuokoa maisha ya kurefusha maisha zinadorora. Idadi ya watu wanaopata matibabu ya VVU ilikua polepole zaidi mnamo mawaka 2021 kuliko ilivyo katika zaidi ya muongo mmoja. Na wakati robo tatu ya watu wote wanaoishi na VVU wanapata matibabu ya kurefusha maisha, takriban watu milioni 10 hawana, na nusu (52%) tu ya watoto wanaoishi na VVU wanapata dawa za kuokoa maisha; pengo la upatikanaji wa matibabu ya VVU kati ya watoto na watu wazima linaongezeka badala ya kupungua. 

Muuguzi akifanya vipimo vya VVU katika Hospitali ya Wau, Sudan Kusini
© UNICEF/Albert Gonzalez Farran
Muuguzi akifanya vipimo vya VVU katika Hospitali ya Wau, Sudan Kusini

Janga la UKIMWI lilichukua maisha, kwa wastani, mnamo mwaka 2021, kulikuwa na  vifo vya UKIMWI 650,000 licha ya matibabu madhubuti ya VVU na zana za kuzuia, kugundua na kutibu magonjwa nyemelezi. 

"Takwimu hizi zinahusu utashi wa kisiasa. Je, tunajali kuwawezesha na kuwalinda wasichana wetu? Je, tunataka kukomesha vifo vya UKIMWI miongoni mwa watoto? Je, tunaweka kuokoa maisha mbele ya kuharamisha?”Aliuliza Byanyima. "Ikiwa tutafanya hivyo, basi lazima turudishe  kwenye mstari mapambano dhidi ya UKIMWI." 

Kulikuwa na tofauti kubwa kati ya nchi. Baadhi ya nchi zilizo na ongezeko kubwa la idadi ya maambukizi mapya ya VVU tangu 2015 ni pamoja na: Ufilipino, Madagascar, Congo na Sudan Kusini. Kwa upande mwingine, Afrika Kusini, Nigeria, India na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilikuwa na upunguaji mkubwa zaidi wa idadi ya maambukizi ya VVU hata wakati wa COVID-19 na majanga mengine. Mifano ya maendeleo inaelekeza kwenye kile ambacho mwitikio unaofaa wa janga unahitaji - kukiwa na baadhi ya maendeleo yenye nguvu ambapo huduma zinazoongozwa na jamii, kuwezesha mazingira ya kisheria na kisera, na huduma zinazolingana ziwe wazi zaidi.