Jamii ina nafasi kubwa katika kutokomeza UKIMWI- UN

1 Disemba 2019

Leo ni siku ya Ukimwi duniani maudhui yakielekezwa katika nafasi ya jamii katika kufanikisha vita dhidi ya kuenea kwa Virusi Vya Ukimwi, VVU na Ukimwi.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa jamii hiyo ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia na wanaharakati ambapo katika ujumbe wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema juhudi endelevu za pamoja ndio muarobaini wa kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

“Umoja wa Mataifa, serikali, asasi za kiraia na washirika wengine wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja kuongeza kasi ya mchakato wa huduma za afya na kukomesha maambukizi mapya ya VVU,” amesema Guterres.

Na ni kutokana na umoja na mshikamano katika vita dhidi ya Ukimwi ndio maana Katibu Mkuu anasema kuwa tayari matunda yameanza kuonekana kwa sababu, “zaidi ya watu milioni 23 wanaoishi na VVU walipatiwa matibabu mwaka 2018.Jamii kote duniani ziko katika kitovu cha hatua hizi, kusaidia watu kudai haki zao, kuchagiza fursa za kupata huduma za jamii na za afya zisizo na unyanyapaa , kuhakikisha kwamba huduma zinawafikia wale wanaozihitaji zaidi na waliotengwa na kushinikiza kubadilisha sheria ambazo zinabagua kama yanavyoainisha mauadhui ya siku ya mwaka huu , jamii zinaleta mabadiliko.”

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema bado kuna mahitaji ambayo hajatimizwa, kwa kuwa kuna watu milioni 38 wanaoishi na VVU hivi sasa na rasilimali za kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi zilipungua kwa dola bilioni 1 mwaka jana.

Mashine kwa udhamini wa Global Fund ili kupambana na VVU, Kifua Kikuu na Malaria inawasaidia maafisa wa afya wa gereza la Pollsmoor Afrika Kusini kuwapima na kuwatibu wafungwa
Photo: The Global Fund/John Rae
Mashine kwa udhamini wa Global Fund ili kupambana na VVU, Kifua Kikuu na Malaria inawasaidia maafisa wa afya wa gereza la Pollsmoor Afrika Kusini kuwapima na kuwatibu wafungwa

Amesisitiza kuwa sasa kuliko wakati mwingine wowote “tunahitaji kukumbatia jukumu la mashirika yanayoongozwa na jamii ambayo yanapigania wenzao, yanayopeleka huduma za VVU, yanayotetea haki za binadamu na kutoa msaada.”

Amesema mahali ambako jamii zimehusishwa mabadiliko yakitokea, uwekezaji ukitoa matokeo na pia usawa, heshima na utu vimekuwepo. Tayari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati jamii imeshaanza kuchukua hatua.

Akiunga mkono kauli hiyo ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na ukimwi UNAIDS Winnie Byanyima amesema kwa kupitia jamii dunia inaweza kutokomeza ukimwi.

“Nina imani na jamii, jamii zinaleta mabadiliko, jamii ndio matumaini yetu makubwa ya kutokomeza ukimwi , kwa sababu jamii zimepambana dhidi ya HIV tangu mwanzo,” amesema Bi. Byanyima.

Na amesema bila jamii “watu milioni 24 wasingekuwa katika matibabu leo hii, bila jamii zinazoongozwa na wanawake wanaoishi au kuathirika na VVU tusingekaribia kukomesha maambukizi mapya miongoni mwa watoto, na kulea yatima pamoja na kuhudumia wagonjwa.”

Hata hivyo amehimiza juhudi zaidi katika vita hivi ikizingatiwa kwa mwaka 2018 watu milioni 1.7 walipata maambukizi mapya ya VVU, watu milioni 37.9 walibainika kuishi na VVU na watu 770,000 walikufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na ukimwi.

 

VVU si hukumu ya Kifo- Doreen

Doreen Moraa Moracha, msichana kutoka Kenya ambaye anaishi na Virusi Vya Ukimwi anajitambulisha kuwa ni mtu mwenye simulizi ya kupendeza kwa kuzingatia kuwa amezaliwa na virusi hivyo na anaishi navyo wa miaka 27 sasa na katu anasema haviwezi kumkwamisha ndoto zake. Doreen ana ujumbe kwa watu wanaoishi na VVU akisema kuwa, “wewe ni zadii ya VVU, unaishi na VVU kwa sababu wewe una nguvu na tambua kuwa Mungu hawezi kukujaribu zaidi ya uwezo wako. Una uwezo wa kukabili unyanyapaa na kuwa shuhuda miongoni mwa jamii na una uwezo wa kusimama na kusema kuwa VVU si hukumu ya kifo. Ujumbe wangu ni kwamba pia jikubali, kunywa dawa.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter