Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Biashara ya huduma kuondoa Afrika kwenye utegemezi wa kilimo na madini- UNCTAD

Spika Janja, spika ya kwanza kabisa janja kutengenezwa barani Afrika
Smart Kaya
Spika Janja, spika ya kwanza kabisa janja kutengenezwa barani Afrika

Biashara ya huduma kuondoa Afrika kwenye utegemezi wa kilimo na madini- UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Eneo la biashara huru barani Afrika linakua, idadi ya watu wenye kipato cha kati inaongezeka, halikadhalika soko la walaji linaibuka sambamba na huduma za kifedha na teknolojia, imesema Kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo, UNCTAD hii leo huku ikitanabaisha kuwa mambo yote hayo ni fursa kubwa kwa Afrika kupanua vyanzo vyake vya kujipatia kipato.

 

UNCTAD katika ripoti yake iliyotolewa leo Geneva, Uswisi, iitwayo Maendeleo ya Kiuchumi Afrika mwaka 2022 inasema kupanua wigo wa vyanzo vya mapato kutasaidia Afrika kuondokana na utegemezi wa mazao ya kilimo na madini katika kujipatia fedha za kigeni.

“Sekta binafsi nayo inakua,” imesema UNCTAD ikiongeza kuwa kupanua wigo wa vyanzo vya mapato kutasaidia bara la Afrika likabiliane na changamoto na majanga makubwa yanayokumba dunia kama vile coronavirus">COVID-19 na vita ya Ukraine.

Jitihada za kupanua wigo wa vyanzo vya kiuchumi bado kuzaa matunda

UNCTAD inasema licha ya juhudi za miongo kadhaa za kupanua wigo wa vyanzo vya bidhaa za kuuza nje ya bara hilo, bado mataifa 45 kati ya 54 yanategemea kilimo na madini pekee.

Kamati hiyo inasema kigezo cha kubaini kuwa nchi inategemea vyanzo hivyo pekee ni pale asilimia 60 ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi zinapokuwa zinatoakana na kilimo na madini.

“Utegemezi wa mazao na madini kwa ajili ya kupata fedha za kigeni utaacha uchumi wa Afrika ukiwa hatarini zaidi pindi majanga yanapotokea na vile vile uchumi jumuishi utasalia ndoto,” amesema Rebeca Grynspan amabye ni Katibu Mkuu wa UNCTAD.

Naomi akiwa kwenye kioski tayari kuchukua fedha taslimu za msaada kutoka WFP
© WFP/Andy Higgins
Naomi akiwa kwenye kioski tayari kuchukua fedha taslimu za msaada kutoka WFP

Amesema Afrika ina uwezo na fursa kubwa ya kuondokana na utegemezi huo na kuhakikisha inajijumuisha kwa ufanisi kwenye minyonyoro ya thamani ya kimataifa.

“Kwa kushughulikia vikwazo vya biashara ya huduma, na kuinua stadi zinazotakiwa pamoja na kuongeza fursa ya ubunifu kwenye mbini mbadala za ufadhili, Afrika inaweza kujitoa kwenye mzunguko wa kutegemea mazao na madini pekee,” ametanabaisha Bi. Grynspan.

Huduma zitakazo ufahamu wa kina

UNCTAD inasema huduma zinazohitaji ufahamu wa juu, kama vile teknolojia ya habari na huduma za kifedha zinaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa Afrika. “Lakini kwa sasa vinachangia asilimia 20 tu ya mauzo ya bidhaa za nje kwa Afrika na hiyo kuengua fursa kubwa ya ukuaji,” imesema UNCTAD.

Kinachoponza Afrika, kwa mujibu wa UNCTAD, ni kwamba sekta ya huduma barani humo imegubikwa na miamala ya kiwango cha chini na hivyo kushindwa kugharimia au kusaidia kukuza sekta za viwanda, uzalishaji na kilimo.

Biashara ya huduma nayo ni ya kiwango cha chini barani Afrika. Kati ya mwaka 2005 na 2017, biashara ya huduma ilichangia asilimia 17 tu ya mauzo ya nje barani Afrika.

Huduma za safari na usafirishaji zilichangia theluthi mbili tu kwenye kiwango hicho na hivyo kudhihirisha ni kwa vipi bado Afrika imejikita kwenye biashara ya huduma zilizozoeleka.

Nini kifanyike?

UNCTAD inasema Afrika iweke será fanisi na thabiti ili kuwezesha mabadiliko hayo ikiwemo será za kupunguza gharama za biashara ya huduma, kuondoka será za kulinda soko na kupanua wigo wa matumizi ya kidijitali sambamba na kuimarisha stadi za wafanyakazi katika sekta ya huduma.