Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika dhibiti utoroshaji fedha upate dola bilioni 89 kila mwaka - Ripoti

Ripoti ya UNCTAD kuhusu maendeleo ya uchumi Afrika inataka udhiibiti wa utoroshaji wa fedha barani humo ambao hupora mitaji yenye thamani ya takribani dola bilioni 89 kila mwaka.
Unsplash/Jason Leung
Ripoti ya UNCTAD kuhusu maendeleo ya uchumi Afrika inataka udhiibiti wa utoroshaji wa fedha barani humo ambao hupora mitaji yenye thamani ya takribani dola bilioni 89 kila mwaka.

Afrika dhibiti utoroshaji fedha upate dola bilioni 89 kila mwaka - Ripoti

Ukuaji wa Kiuchumi

Kila mwaka, takribani dola bilioni 89 hutoroshwa katika nchi za Afrika na kusababisha bara hilo umaskini na kukosa mitaji, imesema ripoti mpya kuhusu maendeleo ya uchumi wa Afrika,  iliyotolewa leo na kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD.
 

Ripoti hiyo iliyotolewa jijini Geneva, Uswisi inasema kuwa kiwango hicho ni saw ana asilimia 3.7 ya pato la ndani la Taifa barani humo.

UNCTAD inaainisha mmiminiko haramu wa fedha au mali kuwa kitendo cha mali au fedha zisizo halai au zilizopatikana kinyume cha sheria kuhamishwa kutoka sehemu moja au nyingine kwa ajili ya matumizi ambapo ripoti iliyotolewa leo inataka kitendo hicho kidhibitiwe ili kuongeza kasi ya maendeleo endelevu Afrika.

Mathalani ripoti inaonesha kuwa mmiminiko huo wa mali na fedha ni takribani sawa na jumla ya kiasi cha fedha za misaada rasmi ya maendeleo ambacho ni dola bilioni 48 na kile cha uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni ambao ni dola bilioni 54 vilivyokuwa vinapatikana kwa wastani kila mwaka kati ya 2013 na 2015.

Kwa Katibu Mkuu wa UNCTAD, Mukhisa Kituyi “Mmiminiko haramu wa fedha na mali unapora bara la Afrika na watu wake matumaini yao, na unakwamisha uawzi na uwajibikaji huku vikimomonyoa imani kwa taasisi za Afrika.”

Akifafanua mmiminiko huo haramu, Kituyi ametolea mfano uhamishaji wa mitaji, ukwepaji wa kodi au makadirio ya chini ya malipo ya kodi ya bidha zinazosafirishwa kwa meli, masoko haramu ya bidhaa, ufisadi na wizi.

Njia ya reli mpya kwenye mgodi  wa  madini nchini Liberia
Picha ya UN/B Wolff
Njia ya reli mpya kwenye mgodi wa madini nchini Liberia

Kati ya  mwaka 2000 na 2015, kiwango cha mitaji iliyoporwa kutoka Afrika kwa njia hizo kilifikia thamani ya dola bilioni 836. “Ikilingaishwa na jumla ya deni la nje la Afrika la mwaka 2018 la dola bilioni 770, kiwango hicho kilichoporwa kinafanya Afrika iwe mkopeshaji mkubwa duniani.”

Sekta ya uziduaji madini inaongoza utoroshaji wa mitaji Afrika

Ripoti inaweka bayana kuwa sekta ya madini ndimo hasa Afrika inapoteza fedha nyingi zaidi kupitia utoroshwaji wa mitaji yake ikieleza kuwa, mwaka 2015 pekee dola bilioni 15 zilipotea.

Katika sekta ya madini, utoroshaji uliongoza katika mnyororo wa thamani wa madini ya dhahabu, ukifuatiwa na almasi na kisha platinum.

UNCTAD inaonya kuwa mimiminiko hii haramu ya fedha ni mwiba kwa Afrika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Mathalani ripoti imebaini kuwa, kwa nchi ambazo kiasi kikubwa cha fedha kinatoroshwa kupitia IFFs, serikali hutumia chini ya asilimia 25 kuliko nchi zingine katika sekta ya afya, elimu chini ya asilimia 58. “Kwa kuwa wanawake na wasichana hawana fursa kubwa ya kupata huduma za afya na elimu, wanakuwa wanadhurika zaidi na mimiminiko haramu ya fedha.”

IFFs na SDGs

Ripoti inasema kuwa Afrika haitaweza kuziba pengo la kufadhili miradi ya SDGs, ambalo ni dola bilioni 200 kila mwaka, kwa kuzingatia mapato ya sasa ya serikali na kiwango kidogo cha misaada rasmi ya maendeleo.

Ni kwa mantiki hiyo ripoti inasisitiza kuwa kudhibiti utoroshaji wa fedha na mitaji, ndio jawabu la kupata mitaji ya kufadhili vitegauchumi muhimu kama vile miundombinu, elimu, afya na kujenga uwezo wa uzalishaji.

UNCTAD imetolea mfano Sierra Leone ikisema kuwa taifa hilo la Afrika Magharibi lenye kiwango cha juu cha vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5, linaweza kuwekeza zaidi kwenye afya na elimu iwapo litadhibiti utoroshaji wa fedha.

Nchini Sierra Leone, katika kila vizazi 1,000 watoto 105 wanafariki dunia, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018, kwa hiyo uwekezaji kwenye afya unaweza kuokoa watoto 2,322 kati ya watoto 258,000 wanaozaliwa kila mwaka nchini humo.

Ripoti inataka watafiti na watunga sera wapate mbinu za kubaini jinsi ya kudhibiti utoroshaji na inapatia serikali ufahamu wa mianya ya kufanyika kwa vitendo hivyo na majawabu ili mapato ya sekta hizo yaelekezwe kwenye utekelezaji wa SDGs.

Hata hivyo inataka juhudi za kimataifa ili kuendeleza ushirikiano wa kimataifa kudhibiti utoroshaji wa fedha na mali.