Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cryptocurrency: UNCTAD yatangaza sera 3 zakufuatwa katika matumizi ya sarafu za kidijitali

Sarafu za kidijitali Crypto currency
Unsplash/Kanchanara
Sarafu za kidijitali Crypto currency

Cryptocurrency: UNCTAD yatangaza sera 3 zakufuatwa katika matumizi ya sarafu za kidijitali

Ukuaji wa Kiuchumi

Kamati ya  Umoja wa Mataifa wa Biashara na Maendeleo UNCTAD imetoa mapendekezo ya sera tatu zinazoweza kutumiwa na nchi zinazoendelea kufuatia kuongezeka kwa matumizi ya sarafu za kidijitali au Cryptocurrency wakati huu ambapo nchi nyingi hazina sera wala mifumo madhubuti ya udhibiti na matumizi yake kwa jamii.

Kamati hiyo ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD inasema, janga la COVID-19 lilivyoibuka duniani na watu kujitenga  ilikuwa vigumu kufanya biashara,  manunuzi na hata utumaji wa fedha kwa familia kutoka nchi moja kwenda nyingine na hivyo njia mbalimbali zilitumika hali iliyofanya hata nchi ambazo hapo awali hazitumii sarafu za kigijitali au Cryptocurrency kuanza kuzitumia. 

Ingawa sarafu hizi ni za kibinafsi zimekuwa na manufaa na kuwezesha hata utumaji wa fedha, ni mali isiyo na utulivu na inaweza kuleta madhara kwa jamii na pia gharama kubwa. 

Ni kwa mantiki hiyo hii leo UNCTAD imetoa miongozo mitatu ya kisera inayomulika hatari hizo ambazo zinaangazia Mosi tisho la sarafu hizo kwenye utulivu wa kifedha, Pili: uhamasishaji wa rasilimali ndani ya nchi na tatu usalama wa mifumo ya kifedha. ufafanuzi wa sera hizo ni kuwa:-

Bitcoin ni miongoni mwa sarafu za kidijitali ambazo unaweza kuuza na kununua au kubadilisha moja kwa moja bila kuhitaji huduma ya kibenki
Unsplash/André François McKenz
Bitcoin ni miongoni mwa sarafu za kidijitali ambazo unaweza kuuza na kununua au kubadilisha moja kwa moja bila kuhitaji huduma ya kibenki

Sio kila king’aacho ni dhahabu

Muhtasari wa sera hii iliyoitwa "Sio yote ambayo yanang’aa ni dhahabu: Gharama kubwa ya kuacha sarafu za kidijitali bila kudhibitiwa" inachambua  sababu za ukuaji wa haraka na kuanza kutumika kwa fedha hizi mtandaoni katika nchi zinazoendelea, ikijumuisha kurahisisha utumaji fedha nje ya nchi na pia kama kizingiti dhidi dhidi ya mfumuko wa bei.

Mishtuko ya hivi karibuni ya sarafu hizi za kidijitali kwenye soko inaonyesha kuwa kuna hatari za kibinafsi za kuzishikilia, lakini ikiwa benki kuu itaingia kati ili kulinda utulivu wa kifedha, basi shida hii inayolikabili soko inakuwa ya umma.

Ikiwa fedha hizi za kidjitali zitasambaa kama njia iliyoenea ya malipo na hata kuchukua nafasi ya fedha za ndani ya nchi kwa njia isiyo rasmi (mchakato unaoitwa cryptoization), hii inaweza kuhatarisha uhuru wa kifedha wa nchi.

Katika nchi zinazoendelea ambazo zina mahitaji ambayo hayajafikiwa ya fedha za akiba, fedha siziso na uimara husababisha hatari fulani. Kutokana na baadhi ya sababu hizi, Shirika la Fedha la Kimataifa IMF limetoa maoni kwamba sarafu za Kidijitali zina hatari kama ilivyo kwa zabuni halali.

Mifumo ya malipo ya umma katika enzi ya kidijitali

Muhtasari wa sera unaoitwa "Mifumo ya malipo ya umma katika enzi ya kidijitali: Kukabiliana na uthabiti wa kifedha na hatari zinazohusiana na usalama za sarafu za kijiditali " inaangazia athari za sarafu hizo kwa uthabiti na usalama wa mifumo ya fedha, na uthabiti wa kifedha.

Inasemekana kuwa mfumo wa malipo wa kidijitali wa nchini ambao hutumika kama manufaa ya umma unaweza kutimiza angalau baadhi ya sababu za matumizi ya crypto na kupunguza upanuzi wa sarafu za kijiditali katika nchi zinazoendelea.

Kulingana na uwezo na mahitaji ya kitaifa, mamlaka za kifedha zinaweza kutoa sarafu ya kidijitali ya benki kuu au, kwa urahisi zaidi, mfumo wa malipo wa haraka wa rejareja. Kwa kuzingatia hatari ya kuzidisha mgawanyiko wa kidijitali katika nchi zinazoendelea, UNCTAD inazitaka mamlaka kudumisha utoaji na usambazaji wa pesa taslimu.

Gharama ya kufanya kidogo na kwa kuchelewa

Muhtasari wa sera unaoitwa "Gharama ya kufanya kazi kidogo sana na kwa kuchelewa: Jinsi fedha hizi za kidijitali zinavyoweza kudhoofisha uhamasishaji wa rasilimali za ndani katika nchi zinazoendelea"  Sera hii imejadili jinsi fedha za kidijitali zimekuwa njia mpya inayohujumu uhamasishaji wa rasilimali za ndani katika nchi zinazoendelea.

Ingawa zinaweza kuwezesha utumaji pesa, zinaweza pia kuwezesha ukwepaji na kuepusha kodi kupitia mtiririko haramu, kana kwamba ni mahali pasipo na kodi ambapo umiliki hautambuliki kwa urahisi.

Kwa njia hii, sarafu za kidijitali zinaweza pia kuzuia ufanisi wa udhibiti wa mitaji, chombo muhimu kwa nchi zinazoendelea kuhifadhi nafasi zao za sera na utulivu wa uchumi mkuu.

Fedha za noti zinachapishwa na serikali
Unsplash/Jason Leung
Fedha za noti zinachapishwa na serikali

Mambo ya kuzingatia wakati wa kutumia sera mpya

Sera hizo tatu kwa pamoja zimeshauri nchi zinazoendelea masuala kadhaa ikiwemo, Kuhakikisha kuna udhibiti kamili wa kifedha wa sarafu zote za kidijitali na kupiga marufuku taasisi za kifedha zinazodhibitokushikilia sarafu pamoja na kushiriki katika biashara ya bidhaa zinazohusiana sarafu hizo. 

Kuzuia matangazo yanayohusiana na sarafu hizo, kutoa mifumo ya malipo kwa umma iliyo salama, inayotegemewa na ya gharama nafuu inayoendana na ulimwengu tuliopo.

Mapendekezo mengine ni kukubaliana na dunia katika uratibu wa kodi na udhibiti na kushiriki katika utoaji wa taarifa na mwisho ni nchi hizo zinazoendelea kuhakikisha zinaweka udhibiti mpya wa mitaji ili kuzingatia vipengele vilivyowekwa na benki kuu za kila nchi, ambavyo havijawekwa na benki kuu na visivyojulikana kutokana na matumizi ya fedha hizi za kimtandao ambazo bado ni mfumo mpya kwa jamii nyingi.