Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 222 sasa wanaishi katika mazingira ya majanga yanayoathiri elimu yao: UNICEF

Shule ya Fugee ambayo ilianzishwa 2009, imetoa elimu kwa takriban wakimbizi watoto 300.
Grace Tan / Payong
Shule ya Fugee ambayo ilianzishwa 2009, imetoa elimu kwa takriban wakimbizi watoto 300.

Watoto milioni 222 sasa wanaishi katika mazingira ya majanga yanayoathiri elimu yao: UNICEF

Utamaduni na Elimu

Mfuko wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu elimu kwenye maeneo yenye dharura na majanga, ECW umetoa ripoti ya kutisha hii leo ikidokeza kuwa idadi ya watoto wenye umri wa kwenda shule, ambao wameathirika na majanga na hivyo kuhitaji msaada  wa kielimu imeongezeka kutoka milioni 75 mwaka 2016 hadi milioni 222 hii leo. 

Mkurugenzi wa mfuko huo Yasmine Sherif, amewaeleza waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi kuwa katika idadi hiyo inayojumuisha watoto na barubaru, milioni 78.2 hawako shuleni, milioni 120 wako shuleni lakini hawapati hata kiwango cha chini cha uelewa wa hisabati au kusoma. Idadi hiyo inamaanisha kuwa ni mtoto 1 kati ya 10 kwenye maeneo hayo ndio ana uwezo wa kufanya hisabati na kusoma. 

Asilimia 84 ya watoto hao wanaishi kwenye maeneo yenye mizozo iliyodumu kwa muda mrefu kama vile Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mali, Nigeria, Sudan Kusini, Sudan na Yemen. 

Mustakbali wao umeporwa

Akizungumzia hali hiyo katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema watoto hao milioni 222 kote duniani elimu yao imeingiliwa na kuvurugwa na zaidi ya hapo “ndoto zao za mustkbali bora zimeporwa na vita, kutawanywa na majanga ya mabadiliko ya tabianchi.”

Ameongeza kuwa katiika wakati wa majanga haya mfuko wa ECW unasimama Pamoja na watoto hao walioko katika nchi 40 duniani.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa “tunazitaka serikali, makampuni ya biashara mifuko mbalimbali ya ufadhili na watu binafsi kuunga mkono na kusaidia kazi muhimu ya ECW.”

Pia amesema mawazo yao na ubunifu wao unahitajika hasa wakati huu wa maandalizi ya mkutano wa mabadiliko ya elimu unaotarajiwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu.

Amehitimisha taarifa yake akitoa rai kwamba “hebu tuhakikishe elimu inaweza kumfikia kila mtoto kila mahali. Hetu tusaidieni kuhakikisha ndoto za watoto hawa milioni 222 zinakuwa hai.”