Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinda amani kutoka Rwanda auawa katika shambulio CAR, UN yalaani

Walinda amani wanaohudumu katika MINUSCA huko CAR wakifanya doria katika mji mkuu Bangui
UN photo / Catianne Tijerina
Walinda amani wanaohudumu katika MINUSCA huko CAR wakifanya doria katika mji mkuu Bangui

Mlinda amani kutoka Rwanda auawa katika shambulio CAR, UN yalaani

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali shambulio liliofanya na wapiganaji wasiojulikana waliokuwa na silaha karibu na mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na kuua na kujeruhi akari wa vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo wakiwemo pia walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake mjini New York Marekani Antonio Guterres amesema shambulio hilo dhidi ya jeshi la ulinzi na vikosi vya usalma vya CAR na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA karibu na Bangui limekatili Maisha ya mlinda amani mmoja kutoka Rwanda na mwinmgine kujeruhiwa.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za mlinda amani aliyepoteza maisha, watu na serikali ya Rwanda na amemtakia ahuweni ya haraka aliyejeruhiwa.

Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu imekumbusha kwamba mashambulizi dhidi ya walindamani wa Umoja wa Mataifa huenda ikawa ni uhalifu wa kivita.

Ametoa wito kwa mamlaka ya CAR kuchukua hatua zote za lazima ili kuhakikisha uwajibikaji kwa mashambulizi haya ya kikatili.

Pia amesema bado anatiwa hofu kubwa na kuendelea kuvurugwa kwa juhudi za kuleta utulivu kunakofanywa na makundi yenye silaha CAR na kutoa wito kwa pande zote kusitisha machafuko na kujihusisha katika majadiliano.

Amepongeza walinda amani wa Umoja wa Mataifa kuendelea kujihusisha kwa karibu na wadau wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika juhudi za kulinda raia na kuleta utulivu wa kitaifa.

Katibu Mkuu amerejelea ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kufanyakazi kwa karibu na washirika wa kitaifa, kikanda na kimataifa kusaidia mchakato wa amani CAR.