Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu za kukabiliana na anguko la kiuchumi zizingatie watu na utu:ILO

Binti Mfanyakazi wa kiwanda cha nguo akitabasamu nyuma ya barakoa yake ya kinga kwa COVID-19, nchini Uturuki
© ILO/Kivanc Ozvardar
Binti Mfanyakazi wa kiwanda cha nguo akitabasamu nyuma ya barakoa yake ya kinga kwa COVID-19, nchini Uturuki

Mbinu za kukabiliana na anguko la kiuchumi zizingatie watu na utu:ILO

Haki za binadamu

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifala Kazi duniani  ILO, Guy Ryder, ameitaka jumuiya ya kimataifa kupunguza kauli zenye maono ya matarajio na badala yake kuchukua hatua za pamoja zinazohitajika kukabiliana na anguko la kijamii na kiuchumi lililosababishwa na janga la COVID-19.

Akifungua Kongamano la ILO la ufufuaji wa uchumi unaozingatia ubinadamu linalofanyika Geneva Uswisi, Ryder amezungumzia kuongezeka kwa pengo kubwa la ukosefu wa usawa.

“Njia tunazotumia sasa hatakama zitasaidia kupunguza pengo hili lakini zinachukua muda mrefu zaidi. Lazima tuchukue hatua ya kubadili muenendo huu duniani vinginevyo itafanya dunia isiwe na haki na hii ni hatari zaidi. “

Ameongeza kuwa “Kwa kujenga mistari mipya na thabiti ya hatua za ushirikiano wa pamoja katika kila maeneo jukwaa hili litakuwa linashughulikia ukuaji unaojumuisha watu wote na na ajira za staha, ulinzi wa kijamii kwa wote, kulinda wafanyakazi na biashara zinazoendelea, na ninjia mojawapo ya kuelekea katika kulinda mazingira- hii italeta mafanikio yanayoonekana.”

Kongamano hilo la siku tatu lilioanza jana na kutarajiwa kukamilika hapo kesho ( 22-24 Februari 2022) limehudhuriwa na wakuu wa nchi na serikali , viongozi wa ngazi za juu wa mashirika ya kimataifa,  viongozi wa waajiri na wafanyakazi kutoka kote ulimwenguni ili kupendekeza hatua madhubuti zitakazoimarisha mwitikio wa kimataifa kwa janga la coronavirus">COVID-19.

Akizungumza katika kikao cha ufunguzi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewaambia wajumbe kwamba Jukwaa hilo kuwa limekuja wakati muhimu ambapo uwezo watu kupona kutokana na janga la COVID-19 na kuokoa Malengo ya Maendeleo Endelevu -SDGs unategemea uwepo wa usawa katika jamii.

“Tunahitaji kurejea kwenye ubinadamu ambao jambo la kwanza la kuzingatia ni kuwaweka watu mbele, [Hii ina maana] kufikia ulinzi wa kijamii kwa wote... njia bora ya ulinzi dhidi ya mishtuko ya kila aina na muhimu kwa mabadiliko ya haki. Inamaanisha uwekezaji wa kimkakati katika ajira zenye staha na kuharakisha urasimishaji wa ajira katika sekta isiyo rasmi. Kuweka watu kwanza kunamaanisha usawa wa kweli wa chanjo... kurekebisha mfumo wa fedha duniani ili nchi zote ziweze kupata ufadhili wa kusaidia watu wao, ikiwa ni pamoja na kupitia msamaha wa madeni na mifumo ya haki ya kodi... ahadi za mabadiliko ya tabianchi zinazolingana na ukubwa na uharaka wa mgogoro.” Amesema Guterres

Wahudhuriaji wa jukwaa hilo wanapata fursa ya kuchunguza hatua na uwekezaji unaohitajika ili kutimiza azma ya wito wa Kiulimwengu wa ILO wa Kufanya Kazi na mchanganuo wa Kimataifa wa Kazi na Ulinzi wa Jamii.