Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna uhusiano kati ya idadi ndogo ya wanawake katika sayansi na kanuni za hovyo za upendeleo wa kijinsia - Guterres 

Msichana akifanya jaribio la kisayansi la kemia katika shule ya sekondari mjini Lusaka, Zambia.
© UNICEF/Karin Schermbrucker
Msichana akifanya jaribio la kisayansi la kemia katika shule ya sekondari mjini Lusaka, Zambia.

Kuna uhusiano kati ya idadi ndogo ya wanawake katika sayansi na kanuni za hovyo za upendeleo wa kijinsia - Guterres 

Wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya viwango vya chini vya wanawake wanaofanya kazi katika masuala ya Akili Bandia (AI), na kanuni za hovyo za upendeleo wa kijinsia ambazo huchukulia wanaume kama watu wa viwango na wanawake kama tu ilimradi. 

Bwana Guterres ameyasema hayo kupitia katika ujumbe wake wa siku hii ya leo ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi akisema kuwa hivi sasa ni mtu mmmoja tu kati ya watafiti watatu wa sayansi na uhandisi ulimwenguni ambaye ni mwanamke na kwamba vikwazo vya kimuundo na kijamii vinazuia wanawake na wasichana kuingia na kuendelea katika sayansi. 

Ameeleza pia kuwa janga la coronavirus">COVID-19 limeongeza zaidi ukosefu wa usawa wa kijinsia, kuanzia kwenye kufungwa kwa shule hadi kuongezeka kwa vurugu na mzigo mkubwa wa huduma nyumbani. 

“Ukosefu huu wa usawa unanyima ulimwengu wetu vipaji na ubunifu mkubwa ambao haujatumiwa. Tunahitaji mitazamo ya wanawake ili kuhakikisha sayansi na teknolojia inafanya kazi kwa kila mtu.” Amesema Bwana Guterres.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihudhuria mkutano wa sayansi,teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) kuhusu programu za kompyuta.
UN Photo/Antonio Fiorente
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihudhuria mkutano wa sayansi,teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) kuhusu programu za kompyuta.
Soundcloud

Hatua za kuchukua 

Aidha Bwana Guterres ameshauri hatua ambazo anaona ni muhimu kuzichukua akisema, kwamba ulimwengu unaweza na ni lazima kuchukua hatua kwa kuwa na sera zinazojaza madarasa na wasichana wanaosoma teknolojia, fizikia, uhandisi, hesabu. 

Pamoja na hatua zinazolenga kuhakikisha fursa za wanawake kukua na kuongoza katika maabara, taasisi za utafiti na vyuo vikuu. 

Kwa dhamira ya kukomesha ubaguzi na mila potofu kuhusu wanawake katika sayansi. 

Na kwa juhudi kali zaidi za kupanua fursa kwa wanawake wa jamii za watu wachache.  

“Haya yote ni muhimu katika uwanja muhimu wa akili bandia.” Amesisitiza.  

Vilevile Katibu Mkuu wa UN ameendelea kusisitiza kuwa dunia inahitaji wanawake zaidi wanaokuza akili bandia ambayo inamuhudumia kila mtu na kufanya kazi kwa usawa wa kijinsia na kwamba inahitaji pia kubadilisha mienendo ambayo inawazuia wanasayansi wanawake wachanga kusoma taaluma ambazo hutusaidia kushughulikia majanga ya tabianchi na mazingira. 

“Nilifundisha uhandisi. Ninajua kutokana na uzoefu binafsi kwamba wasichana na wanaume wana uwezo sawa na wanavutiwa sawa na sayansi, iliyojaa mawazo, na wako tayari kuendeleza ulimwengu wetu mbele.” Ameeleza.  

Pia Bwana Guterres amesema ni lazima tuhakikishe kwamba wanapata fursa sawa za kujifunza na kufanya kazi kwenye uwanja sawa na akasisitiza akisema, “katika Siku hii ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, ninatoa wito kwa kila mtu kuunda mazingira ambapo wanawake wanaweza kutambua uwezo wao wa kweli na wasichana wa leo wanakuwa wanasayansi na wavumbuzi wakuu wa kesho, wakiunda mustakabali mzuri na endelevu kwa wote.”