Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuengua wanawake kwenye sayansi ni sawa na kukwamisha Ajenda 2030- Guterres

Kundi la wasichana wa Namibia ambao walishiriki katika kambi ya mafunzo ya programu za Kompyuta (AGCC) mjini Pretoria, Afrika Kusini.
UN Namibia
Kundi la wasichana wa Namibia ambao walishiriki katika kambi ya mafunzo ya programu za Kompyuta (AGCC) mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Kuengua wanawake kwenye sayansi ni sawa na kukwamisha Ajenda 2030- Guterres

Wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kusongesha usawa wa jiinsia katika nyanja ya sayansi na teknolojia ni muhimu kwa ajili ya kujenga mustakabali bora zaidi.
 

Guterres amesema hayo katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana kwenye sayansi akiongeza kuwa hali hiyo imekuwa dhahiri wakati huu wa vita dhidi ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.
“Wanawake ni asilimia 70 ya wahudumu wa afya, na wamekuwa ndio waathirika wakubwa zaidi na janga hili na miongoni mwao wanaongoza harakati dhidi ya janga hilo. Ukosefu wa usawa jinsia umeongezeka kwa kiasi kikubwa mwaka uliopita, ambapo wanawake ndio wanabeba mzigo mkubwa zaidi wa shule kufungwa na kufanyia kazi nyumbani, amesema Katibu Mkuu.

Amesema kutokana na janga la Corona, wanawake wengi wanashuhudia kufungwa kwa maabara na kuongezeka kwa wajibu wao wa malezi, huku wakiwa hawana muda wa kutosha kufanya tafiti muhimu.
“Kwa wanawake wanasayansi, changamoto hizi zimeongezeka katika mazingira ambayo tayari hali ilikuwa ni ngumu”
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, wanawake ni theluthi moja tu ya watafiti wote duniani na wanashika nyadhifa chache andamizi kuliko wanaume kwenye Vyuo Vikuu vya hali ya juu.
Katibu Mkuu amesema tofauti hiyo imesababisha kuwepo kwa kiwango kidogo cha machapisho yao, wasionekane vya kutosha na hata kutambuliwa na zaidi ya yote, fedha ni kidogo.

Akili Bandia

Katibu Mkuu amesema akili bandia na kujifunza kwa njia ya mashine vimeongeza wigo wa upendeleo. Amesema ingawa wanawake na wasichana nyanja ya sayansi ni yao bado kuna fikra potofu zinazochochea wanawake na wasichana wakwepe nyanja hiyo.
“Ni wakati wa kutambua kuwa tofauti kubwa huchochea ubunifu mkubwa. Bila kuwa na wanawake kwenye Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu  au STEM, dunia itaendelea kuwa na ubunifu kutoka kwa wanaume, na uwezo wa wanawake na wasichana utasalia kufichika na bila kutumika,” ameonya Katibu Mkuu.
Amesema ni lazima kuhakikisha wasichana wana fursa ya elimu wanayopaswa kuwa nayo na wanajiona kwenye mustakabali wautakao wenyewe iwe uhandisi, programu za kompyuta, teknolojia ya roboti au hata sayansi ya afya.

Guterres amesema hiyo ni kazi muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, akisema, “kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye STEM unaweza kupunguza pengo la malipo ya ujira na kuongeza mapato ya wanawake kwa dola bilioni 299 katika miaka 10 ijayo.”

Stadi za STEM pia ni muhimu katika kupunguza pengo la matumizi ya intaneti duniani na kwamba, “kwa pamoja hebu tutokomeza ubaguzi wa kijinsia na kuhakikisha kila mwanamke na mtoto wa kike anakidhi ndoto zake na anakuwa sehemu muhimu ya kujenga dunia bora zaidi kwa kila mtu.”
Tuzo ya L'Oréal
Katika hatua nyingine lakini iendanayo na siku ya leo, UNESCO na mfuko wa L'Oréal wamepatia tuzo wanawake watano watafiti katika nyanza za hesabu, fizikia, kemia, na mawasiliano ya kimitambo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya tuzo ya 23 ya kimataifa kwa wanawake katika sayansi.
Katika chapisho lake jipya kuhusu usawa wa jinsia kwenye utafiti, UNESCO inaonesha kuwa ijapokuwa idadi ya wanawake kwenye utafiti wa sayansi imeongezeka, bado ni wachache katika nyanja za hesabu, sayansi ya kompyuta, uhandisi na akili bandia.
“Haitoshi kuwavutia wanawake kwenye nyanja ya sayansi au teknolojia, tunapaswa pia kuhakikisha wanabakia humo na kuhakikisha ajira zao hazikumbwi na vikwazo na kwamba mafanikio yao yanatambuliwa na kuungwa mkono na jamii ya kimataifa ya sayansi,” amesema  Shamila Nair-Bedouelle, Mkurugenzi Msaidizi, UNESCO.

TAGS: COVID-19, UNESCO, Siku za UN, STEM