Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kulikoni harakati za kutokomeza ukoloni zimedorora?

Sherehe za maadhimisho ya uhuru wa Timor-Letse mwaka 2020 ambazo zilifanyika katika mji mkuu Dili.
UN Photo/Sergey Bermeniev
Sherehe za maadhimisho ya uhuru wa Timor-Letse mwaka 2020 ambazo zilifanyika katika mji mkuu Dili.

Kulikoni harakati za kutokomeza ukoloni zimedorora?

Masuala ya UM

Maeneo 17 duniani bado yanatawaliwa na harakati za kusaidia maeneo hayo zinaonekana kudorora, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo jijini New York, Marekani wakati akifungua mkutano wa mwaka huu wa 2020 wa kamati maalum kuhusu kutokomeza ukoloni duniani.

Guterres amesema kauli yake hiyo ya kuhoji inazingatia ya kwamba eneo la mwisho kukombolewa kutoka kwenye ukoloni ni Timor Letse na hiyo ilikuwa mwaka 2002.

“Kwa kuzinatia kuwa koloni la mwisho kujikomboa kutoka ukoloni ilikuwa Timor-Letse mwaka 2002, ni vyema kuhoji: Je ajenda ya kutokomeza ukoloni imekumbwa na mkwamo? Jibu ni ‘Hapana.’ Mambo  yanasonga mbele lakini kwa mwendo wa kinyonga,”  amesema Katibu Mkuu.

Mwaka 1947, maeneo 72 yalikuwa kwenye orodha ya wali ya nchi zinazotawaliwa na leo hii zimesalia 17 ambapo Katibu Mkuu amesema “tunapaswa kujivunia mafanikio haya.”

Hata hivyo amesema kuwa Umoja wa Mataifa haupaswi kusahau kuwa wakazi wa maeneo hayo 17 bado wanasubiri ahadi ya kujitawala itekelezwe, kwa mujibu wa Ibara ya XI ya Chata ya Umoja wa Mataifa, Azimio la mwaka 1960 la kupatia uhuru makoloni sambamba na maazimio mengine.

Bwana Guterres amesema kwa kuwa mwaka huu ni  mwaka wa mwisho wa kuadhimisha muongo wa tatu wa kutokomeza  ukoloni ni fursa nzuri ya kutathmini maendeleo ya harakati hizo.

Mara baada ya kupata  uhuru, bendera ya Timor-Letse ilipandishwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini NewYork, Marekani, kuashiria taifa hilo kujiunga na chombo hicho.
UN Photo/Mark Garten)

Amesema mwezi Septemba, eneo la New Caledonia litakuwa na awamu ya pili ya kura ya maoni kuhusu uhuru wake, kufuatia kura ya maoni kama hiyo yam waka 2018.

Halikadhalika, Kamati hiyo ya kutokomeza ukoloni inaendelea kukuza na kujenga uhusiano mpya na maeneo hayo na wale wanaowatawala.

Shaka na shuku za wanaotawaliwa zizingatiwe

Amekumbusha kuwa kutokomeza ukoloni ni mchakato ambao unapaswa kuongozwa na matamanio na mahitaji ya jamii zinazoishi kwenye maeneo hayo.

 “Hofu za wakazi wa makoloni zinatofautiana n ani wajibu wetu kupaza sauti zao. Maeneo mengi yanakabiliwa na changamoto halisi na za dharura. Idadi kubwa na visiwa vidogo vinavyokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Katibu Mkuu akitaja mengine yanahaha kujenga uchumi endelevu na wa kujitegemea.

 “Tunapaswa kuendelea kuwa jukwaa la mashaurino muhimu kati ya maeneo yanayotawaliwa na watawala wao ili kuwezesha wakazi wa maeneo hayo kufanya maamuzi wanayotaka wao kwa ajili ya mustakabali wao,”  amesema Katibu Mkuu.

Je wafahamu maeneo ambayo bado yanatawaliwa?

Hadi sasa maeneo 17 yanayotawaliwa ni, Sahara Magharibi, Anguilla, Bermuda, visiwa vya British Virgn, visiwa vya Cayman, visiwa vya Falklands, Montserrat, Saint Helena, visiwa vya Turks na Caicos, visiwa vya Virgin Marekani, Gibraltar, American Samoa, French Polynesia, Guam, New Caledonia, Pitcairn na Tokelau.