Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilivutiwa kuwa daktari kwa kuzingatia mahitaji ya wasomali-Dkt. Mohamud

Changamoto katika sekta ya afya na namna ambavyo watu walikuwa wakiteseka na upungfu wa wataalam wa afya vilimsukuma Abdulkadir Farah Mohamud kusomea udaktari na kuchangia katika ujenzi wa nchi yake
UNSOM/ Video Capture
Changamoto katika sekta ya afya na namna ambavyo watu walikuwa wakiteseka na upungfu wa wataalam wa afya vilimsukuma Abdulkadir Farah Mohamud kusomea udaktari na kuchangia katika ujenzi wa nchi yake

Nilivutiwa kuwa daktari kwa kuzingatia mahitaji ya wasomali-Dkt. Mohamud

Amani na Usalama

Wakati hali ya utulivu inaendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini Somalia, raia mbalimbali wa taifa hilo walioko ndani na nje ya nchi wanaelekeza juhudi zao katika kuchangia na kukuza ustawi wa jamii kwa njia moja au nyingine. Miongoni mwao ni AbdulKadir Farah Mohamud kama anavyosimulia Grace Kaneiya.

Hii ni sauti ya daktari Abdulkadir Farah Mohamud al maarufu Dkt. Hajji mkazi wa wilaya ya Hodan kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Yeye alikuwa akifanya kazi ugenini kama daktari wa watoto lakini sasa amerejea nyumbani na anafanya kazi katika hospitali ya Kalkal nchini Somalia, katika harakati za kujenga upya taifa lake.

Daktari huyo ni miongoni mwa watu ambao wamemulikwa katika mfululizo wa makala kwa jina ‘sauti za wasomali’. Dkt. Hajji anaelezea kilichomvutia kuwa daktari.

“Nilivutiwa kuwa daktari kwa kuzingatia mahitaji ya wasomali na changamoto katika sekta ya afya na namna ambavyo watu walikuwa wakiteseka na upungfu wa wataalam wa afya. Hapo nilianza kupenda kazi hiyo na nikajitizama kama mtu ambaye anaweza kuleta mabadiliko hapo baadaye.”

Ili kutimiza ndoto zake Dkt. Hajji alikwenda ughaibuni kusoma na alipohitimu alipata kazi. Hata hivyo hali ya nchi yake na mateso waliyokuwa wakipitia wasomali wenzake nchini mwao vilimsukuma kurudi nyumbani ambapo anasema

“Kazi ambayo ninaifanya inachangia kwa kiasi kikubwa katika jamii, niliporejea nyumbani nilianza kufanya kazi  katika hospitali hii. Nilianzisha pia mfuko wa hospitali ya Kalkal ambalo ni shirika la kutoa misaada.”

Daktari huyo anasema pia anatumia muda wake kufanya kazi za kujitolea.