Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upatikanaji wa mafuta na gesi Kenya ni fursa, lakini yenye athari kwa mazingira:UNEP

Pampu za mafuta.Picha: World Bank/Gennadiy Kolodkin (file)

Upatikanaji wa mafuta na gesi Kenya ni fursa, lakini yenye athari kwa mazingira:UNEP

Ukuaji wa Kiuchumi

Matumaini ya Kenya na wananchi wake kujikomboa kiuchumi yanazidi kuongezeka hasa baada ya serikali ya nchi hiyo kutangaza mwaka 2012 kwamba wamegundua mafuta na gesi kwenye kisima cha Ngamia-1 kaunti ya Turkana Kaskazini mwa nchi hiyo.

 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira UNEP uvumbuzi huo unatoa fursa kubwa za maendeleo ya kiuchumi kwa Kenya na mataifa mengine lakini pia unaambatana na athari lukuki hasa kwa mazingira na afya, na kwa kulitambua hilo serikali inataka kuweka mipango ya udhibiti.

UNEP inasema mafuta na gesi ni moja ya watoaji wakubwa wa gesi chafuzi za viwandani hususan aina ya methane ambayo hatari yake ni mara 84 zaidi ya hewa ya ukaa au Carbon Dioxide.

 

Maeneo ya vinamasi hufanya kama "godoro" la kufyonza  hewa ya ukaa kutoka hewani
Photo: UNEP GRID Arendal/Steven Lutz
Maeneo ya vinamasi hufanya kama "godoro" la kufyonza hewa ya ukaa kutoka hewani

 

Na hata kama nchi na jumuiya ya kimataifa wanabadilika na kuelekea katika uzalishaji wa kiwango kidogo cha hewa ya ukaa na uchumi unaojali mazingira, bado mahitaji ya nishati ya kimataifa yatabaki kutegemea mafuta kwa angalau miongo mitatu ijayo.

Mafuta na gesi nchini Kenya imebainika baada ya juhudi za utafiti wa muda mrefu zilizoanza miaka ya 1950 wakati kampuni ya petroli ya Uingereza (BP) na Shell walipochimba visima kadhaa kwenye pwani ya bonde la Lamu .

Image
Picha:Idhaa ya Kiswahili/John Kibego
Uchimbaji wa mafuta Buliisa Uganda.Nayo Kenya inafanya vivo hivyo sehemu za Turkana(Picha:Idhaa ya Kiswahili/John Kibego)

 

Sekta hiyo ya mafuta na gesi ya Kenya inakabiliwa na changamoto nyingi za udhimiti wa mazingira ambazo zinajumuisha uwezo wa kitaasisi, miundombinu, fedha, fursa za ardhi, masuala ya kisheria na mifumo ya ufuatiliaji.

Mei mwaka 2018, UNEP kwa msaada kutoka serikali ya Norway iliandaa mafunzo ya siku nne ili kuchagiza na kupazia sauti uhifadhi wa mazingira katika uchimbaji na uzalishaji wa mafuta na gesi kwa ajili ya maafisa wa serikali ya Kenya, wawakilishi kutoka asasi za kiraia na sekta binafsi.

 

Image
Kenya katika kaunti ya Turkana. Picha: UM/Video capture

Maafisa kutoka wizara mbalimbali, mashirika ya kitaifa na serikali za majimbo walishiriki mafunzo hayo. Lengo kuu la mafunzo hayo ilikuwa ni kuongeza uelewa wa washiriki kuhusu uchimbaji na uzalishaji wa mafuta na gesi na kuwaelimisha athari zake kimazingira.

Tangu mwaka 2016 UNEP na serikali ya Norway wamekuwa wakishirikiana kuimarisha udhibiti wa mazingira katika sekta za mafuta na gesi katika nchi 14 ikiwemo Kenya.