Kama walivyo binadamu wanaocheza filamu , wanyama wanastahili kulipwa wanapohusishwa: UNDP
Wanyama wanahusihwa kwa asilimia 20 kwenye matangazo ya biashara na hata filamu, lakini hawalipwi ujira wowote au kupewa msaada wanaouhitaji, sasa umewadia wakati wa kuwatendea haki.
Kauli hiyo imetolewa na balozi maalum wa mpango wa kuwasaidia na kuwalinda Wanyama ujulikanao kama Lions Share , Sir David Attenborough wakati wa uzinduzi wa wakfu maalumu kwa fuko maalum la ubia kati ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP, muanzilishi wa wakfu huo FINCH na muanzilishi mwenza MARS kwa lengo la kukabiliana na changamoto zilizopo katika uhifadhi wa wanyama pori na maslahi ya wanyama kwa jumla.
(SAUTI YA SIR DAVID ATTENBOROUGH)
“Wanyama ni sehemu ya dunia yetu, utamaduni wetu , jamii yetu pamoja na lugha zetu na hata pia utengenezaji na usambazaji wa filamu. Na kwa kweli picha za wanyama huonekana katika matangazo kwa asilimia 20. Licha ya hivyo, kwa kawaida wanyama hawapatiwi msaada wanaouhitaji mpaka sasa.”
Kupitia mfuko huo, washirika watachangia asilimia 0.5 ya matangazo yake kwa kila tangazo ambalo myama au Wanyama watahusishwa. Pesa hizo zitatumiwa kusaidia mahitaji ya wanyama na makazi yao duniani kote. MARS ndio mshirika wa kwanza wa matangazo katika mpango wa Lions Share.
Sir David anasema ingawa kiwango hicho ni kidogo lakini haba na haba hujaza kibaba
(SAUTI YA SIR DAVID ATTENBOROUGH)
“ Ingawa asilimia 0.5 inaonekana kama pesa ndogo, lakini endapo watangazaji 10 wakuu duniani wataukubali mpango huu, itamaanisha ni mchango wa kila mwaka wa dola milioni 47.”
Hata hilo lengo lao ni kiasi gani ?
(SAUTI YA SIR DAVID ATTENBOROUGH)
“ Lengo letu ni kukusanya dola milioni 100 kila mwaka. Kwa kufanya kitu kidogo leo tuna nafasi kubwa ya kubadili mambo kesho.”
Naye mkuu wa UNDP, Achim Steiner, amesema wanyama pori na makazi yao wako hatarini. Ameongeza kuwa, “tunapoteza aina mbalimbali za wanyama kwa kasi ambayo inakadiriwa kufika mara 1,000 zaidi ya kawaida.” Hivyo mkakati wa Lion’s share ni wazo zuri ambalo litaleta msukumo kuhusu mustakabali wa wanyama, makazi yao na pia ulimwengu wetu.