Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kakuma yawa mwenyeji wa jukwaa la kwanza la kimataifa la TEDx kwenye kambi ya wakimbizi:UNHCR

Mtoto mvulana akiwa pekupeku ambaye ndio amewasili tu kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kaskazini Magharibi mwa Kenya kutokea Sudan Kusini akiwa na sanduku lake kichwani akijaribu kuwahi utaratibu wa kuandikisha wakimbizi
OCHA/Gabriella Waaijman
Mtoto mvulana akiwa pekupeku ambaye ndio amewasili tu kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kaskazini Magharibi mwa Kenya kutokea Sudan Kusini akiwa na sanduku lake kichwani akijaribu kuwahi utaratibu wa kuandikisha wakimbizi

Kakuma yawa mwenyeji wa jukwaa la kwanza la kimataifa la TEDx kwenye kambi ya wakimbizi:UNHCR

Amani na Usalama

Jukwaa la kwanza la kimataifa la TEDx kwa wakimbizi limefanyika Jumamosi kwenye kambi kubwa ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya

Burudani iliyoambatana na ujumbe mahsusi ni moja ya vivutio vilivyotamalaki kwenye jukwaa hilo la kihistoria kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma iliyoko Kaskazini Magharibi mwa Kenya.


Kundi hili ni la vijana wawili wanaojiita Street Boys, ni wakimbizi kutoka Sudan Kusini kambini hapo wenye vipaji vya kuimba muziki wa kufokafoka almaarufu kama Rap.


Jukwaa hilo limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, watu maarufu, mashirika na wahudumu wa misaada, asasi za kiraia, wanaharakati na wahusika wakuu ambao ni  wakimbizi wa sasa kambini hapo na wale waliowahi kuwa wakimbizi ambao hivi sasa maisha yao yamebadilika na kuwa hamasa kwa wengine . 


Miongoni mwa wazungumzaji wakuu katika tukio hilo ni Mary Nyiriak Maker mkimbizi wa zamani kutoka Sudan Kusini ambaye sasa ni mwalimu  anafundisha kambini Kakuma , msichana huyo mwenye umri wa miaka 22 anasema amerejea kambini hapo kwa matumaini ya kuhamasisha vijana

TEDEx/UNHCR
Mary Nyiriak Maker - TEDx Kakuma Camp Promo Video


(SAUTI YA MARY NYIRIAK MAKER)
“Naangalia idadi ya watu kambini hususan idadi ya vijana wngi wao hawana matumaini, na wakiniona mimi mwalimu wao ambaye karibu ni wa rika lao kutawatia matumaini ya kusonga mbele, kuongeza bidi na kuona kwamba maisha sio kuhusu kambi, maisha ni kitu kingine Zaidi kilicho mbele na hicho ndicho ninachotaka waamini” 


Lengo kuu la jukwaa hili ni kubadilishana uzoefu katika juhudi za kubadili hisia na  mtazamo hasi wa kimataifa kuhusu wakimbizi , lakini pia wakimbizi hao kuelezea hadithi zao za mnepo baada ya kupitia changamoto nyingi na ubunifu uliowafanya leo hii kubadili maisha yao na hata kuwa chanzo cha wengine kufuata nyayo zao.

Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR na mmoja wa walioendesha jukwaa hilo amezungumzia mtazamo kuhusu wakimbizi

 

Msemaji wa UNHCR Melissa Fleming
Picha na UNHCR/Jean-Marc Ferré
Msemaji wa UNHCR Melissa Fleming


(SAUTI YA MELISSA FLEMING)


“Watu wengi wa Ulaya, Australia na Marekani wanafikiri kwamba wakimbizi wote wanaelekea kwenye nchi zao, lakini ukweli ni kwamba wengi wao wako katika nchi za Afrika kama Kenya na hawaonekani, tunatumai tukio hili litaiangaza kambi, lakini pia wakimbizi, talanta zao na mawazo yao kwa kuwaweka katika jukwaa lenye nguvu kama hili la TEDx.”


Watu wengine mbalimbali walipata fursa ya kusimulia hadithi zao katika jukwaa hilo akiwemo mwanariadha nyota Yiech Pur Biel aliyewakilisha timu ya kwanza kabisa ya wakimbizi kwenye Olimpiki mwaka 2016 na mlimwende wa Marekani mwenye asili ya Kisomali Halima Aden ambao walikulia kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma.

Hao ni baadhi tu miongoni mwa wanamuziki, washairi, wabunifu wa mitindo, wafanyabiashara na wengineo waliofanikiwa baada ya kuwa wakimbizi.

Mwana Olimpiki Yiech Pur Biel, mkimbizi Raia wa Sudan Kusini , akiwa nchini Korea Kusini alikohudhuria hafla ya kamati ya kimataifa ya Olimpiki
UNHCR/H.Shin
Mwana Olimpiki Yiech Pur Biel, mkimbizi Raia wa Sudan Kusini , akiwa nchini Korea Kusini alikohudhuria hafla ya kamati ya kimataifa ya Olimpiki


Tukio hili la kwanza kwenye kambi ya wakimbizi limefanikishwa kwa msaada wa wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNHCR, UNICEF na Bank ya Dunia, lakini pia kwa mchango wa serikali ya Kenya , Marekani , NGO’s, makapuni binafsi na jumuiya za kimataifa ikiwemo Muungano wa Ulaya.


Kambi ya Kakuma ilianzishwa mwaka 1992 lengo lake la awali likiwa kuhifadhi wakimbizi wa Sudan, lakini hivi sasa ina wakimbizi takribani 186,000 kutoka mataifa zaidi ya 14 bararani Afrika. Kambi hiyo ina shule , vyuo vikiwemo vyuo vikuu na shughuli mbalimbali za kibiashara. 


Mwaka huu ripoti ya Bank ya Dunia na UNHCR  ya mwezi Mei imekadiria kwamba uchumi utokanao na sekta isiyorasmi kambini Kakuma una tahamani ya dola milioni 56.