Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma kwa wajawazito zizingatie mahitaji ya kila mtu- WHO

Mama na mwanae mchanga wakipata huduma baada ya kujifungua kwenye wodi ya wazazi iliyoko kliniki ya Shakawe nchini Botswana.
UNICEF/Christine Nesbitt
Mama na mwanae mchanga wakipata huduma baada ya kujifungua kwenye wodi ya wazazi iliyoko kliniki ya Shakawe nchini Botswana.

Huduma kwa wajawazito zizingatie mahitaji ya kila mtu- WHO

Afya

Shirika la afya duniani, WHO linasema kila mzazi anakuwa na uchungu tofauti wakati anakaribia kujifungua hivyo watoa huduma wahakikishe kuwa huduma hizo zinazingatia mahitaji ya kila mtu badala ya kutumia aina moja ya huduma kwa watu wote.

Tunahitaji wanawake wajifungue katika mazingira salama, wakisaidiwa na wauguzi wenye ujuzi katika vituo vya afya vilivyo na vifaa vyote vinavyohitajika.

Hayo yamesemwa leo na shirika la afya ulimwenguni WHO katika muongozo mpya lililoutoa wa mapendekezo ya kuanzisha viwango vya kimataifa vya huduma kwa kina mama wajawazito wasio na matatizo yoyote na kupunguza kuwapa usiyohitajika wakati wa kujifungua.

Hata hivyo Dkt. Princess Nothemba Simelela mkurugenzi msaidizi wa WHO kwa masuala ya familia, wanawake, watoto na barubaru amesema ongezeko la matumizi ya madawa katika mchakato wa kujifungua kawaida , linaathiti uwezo wa mwanamke wa kujifungua na pia uzoefu wake katika kitendo hicho.

Na kuongeza kuwa

(SAUTI YA DKT PRINCESS SIMELELA)

“Endapo uchungu unaendelea kawaida na mama na mwanae wako katika hali nzuri , hawahitaji kupata usaidizi wa dawa za  kuongeza kasi ya uchungu.”

Muongozo huo mpya wa WHO unatambua kwamba kila uchungu na kila kitendo cha kujifungua ni tofauti kwa kila mama, hivyo katika kupunguza usaidizi wa dawa kwa kina mama wakati wa kujifungua , muda unaotumika wakati mama akiwa katika uchungu hadi wakati anapojifungua usitumike kama kigezo cha kumpa mama dawa za kuongeza kasi ya uchungu au kutaka kumzalisha mapema.

Pia muongozo unasemna kina mama wengi wanataka kujifungua kawaida na wanapendelea kutumia uwezo wa mwili wao kujifungua badala ya kupewa usaidizi wa dawa.
Duniani kote inakadiriwa kuna matukio milioni 140 ya kujifungua kila mwaka na asilimia kubwa hufanyika bila matatizo yoyote kwa kina mama na watoto. Lakini katika miaka 20 iliyopita wauguzi wameongeza matumizi ya madawa ambayo siku za nyuma yalitumika tuu kuepusha hatari au kuzuia matatizo  kwa mtoto au mama na hivyo kuongeza kasi ya uchungu au kufanya upasuaji.

Sasa WHO inataka madaktari na wauguzi kuwashauri kina mama wajawazito wasio na matatizo kuwa muda wa uchungu unatofautina kwa kila mama na mara nyingine kujifungua hakutabiriki.