Radio haitokufa, na inaendelea kuwa na umuhimu mkubwa: IOM

13 Februari 2018

Baadhi ya watu wamekuwa wakidai Radio ni chombo cha habari kinachokufa , lakini ukweli ni kwamba Radio imezidi kushamiri na itaendelea kuwa chombo muhimu cha mawasiliano katika jamii ndani na nje ya masuala ya kibinadamu.

Kauli hiyo imetolewa na afisa mkuu wa mawasiliano wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, bwana Mark Doyle , katika kuadhimisha siku ya Radio hii leo mjini Geneva Uswis, ambako shirika hilo limeandaa shughuli maalumu kwa ushirikiano na mtandao wa mawasiliano ya athari za majanga (CDAC)

Hafla hiyo iliyopewa kichwa “Radio ni uti wa mgongo wa mafanikio katika mazingira ya sasa ya teknolojia ya mawasiliano” imejikita katika mambo mawili, mosi kutanabaisha uhusiano uliopo baina ya matumizi ya radio na afya katika jamii zilizoathirika na majanga, na pili ni jumukumu muhimu la radio kwa jamii zinazohama au kukimbia vita na majanga mengine.

Akitoa mfano amesema kwenye migogoro ya vita kama Somalia na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Radio imekuwa na mchango mkubwa katika kazi za IOM kufikisha msaada na kuwafikia wahitaji ambako vyombo vingine vya habari kama tlevision, magazeti au mtandao wa interneti haufiki.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud