Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wabonga bongo kwa ajili ya amani ya kudumu Somalia

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating (wa pili kutoka kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ulinzi wa raia wa Somalia.
UN Photo/Omar Abdisalan
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating (wa pili kutoka kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ulinzi wa raia wa Somalia.

Wataalamu wabonga bongo kwa ajili ya amani ya kudumu Somalia

Mkutano wa siku tatu unaongazia jinsi ya kuchagiza amani nchini Somalia umeingia siku ya pili hii leo huku Umoja wa Mataifa ukitaka washiriki wabonge bongo ili kumaliza changamoto zinazokabili nchi hiyo. 

Ukileta pamoja washiriki zaidi ya 30 wakiwemo wataalamu, watafiti na wasomi, mkutano huo unalenga kuibuka na chombo cha kitafiti kuhusu jinsi ya  kuzuia mizozo ili hatimaye kuchagiza maridhiano.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating amesema

(Sauti ya Michael Keating)

“Wote wamekusanyika hapa kwa dhati kabisa kubadilishana ufahamu wao, uzoefu na utaalamu. Lengo ni hatimaye kutatua changamoto zinazokumba Somalia na hata wao wenyewe, na hatimaye kujaribu kupunguza kiwango cha ghasia na kusongesha maridhiano ya kitaifa na kadhalika. Pia kuelewa mienendo ya mzozo kwa njia ambayo kwayo itasaidia ninyi na sisi pia katika kusongesha mbele wasomali.”

Kwa upande wake waziri wa Somalia anayehusika na mambo ya ndani, shirikisho na maridhiano, Abdi Mohamed Sabriye amesema serikali yao imeazimia kufanikisha amani ya kudumu na amekaribisha mchango wa wataalamu hao waliokusanyika kwa lengo hilo la amani ya kudumu.

Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano baina ya serikali ya Somalia,  Umoja wa Mataifa kupitia ujumbe wake nchini Somalia, UNSOM pamoja na serikali ya Norway.