Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 3.2 zahitajika kwa wakimbizi wa Sudan Kusini

Mgao wa chakula katika kambi ya Kakuma.(Picha:WFP/Martin Karimi)

Dola bilioni 3.2 zahitajika kwa wakimbizi wa Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na usaidizi wa kibinadamu na wakimbizi leo wametembelea kambi ya Kakuma nchini Kenya ili kushuhudia hali halisi ya kibinadamu wanayokabiliana nayo wakimbizi wa Sudan Kusini nchini humo.

Mark Lowcock wa OCHA na Filipo Grandi wa UNHCR wamepata fursa ya kuzungumza na wakimbizi ambapo mzozo wa Sudan Kusini ukiingia mwaka wa tano bado hakuna matumaini.

Lowcock amesema mamilioni wamekimbia kuokoa maisha yao akipongeza hatua ya Kenya ya kuwapatia hifadhi wakimbizi hao huku akitaka usaidizi zaidi kwa wakimbizi hao.

Kwa mantiki hiyo ametangaza ombi la zaidi ya dola bilioni Tatu kwa mwaka huu wa 2018 ili kusaidia wakimbizi hao ambao idadi yao itafikia zaidi ya milioni tatu mwaka huu na kufanya Sudan Kusini kuwa janga kubwa zaidi la wakimbizi Afrika baada ya lile la Rwanda.

Mchanganuo wa fedha hizo ni kwamba dola bilioni 1.5 ni kwa ajili ya raia wanaokimbia Sudan Kusini ilhali dola bilioni 1.7 ni kwa wakimbizi wa ndani takribani milioni Saba.

Raia wa Sudan Kusini wamesaka hifadhi Uganda, Kenya, Sudan, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.