Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wengi wakimbia mapigano mapya Mashariki mwa DRC—UNHCR

Wengi wakimbia mapigano mapya Mashariki mwa DRC—UNHCR

Mapigano mapya kati ya jeshi la serikali na waasi huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC yamesababisha maelfu ya watu kukimbia kutoka makazi manne ya muda ya hifadhi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema kati ya mwezi Machin a wiki iliyopita watu 36,000 wamekimbia vituo vya hifadhi vya Mpati, Kivuye, Nyange na Bweru huko wilaya ya Masisi, jimbo la Kivu Kaskazini.

Mwakilishi wa UNHCR kwenye ukanda huo Stefano Severe amesema hali hiyo inatia hofu sana ustawi wa watu na hivyo wameomba mamlaka za serikali na pande kinzani kuhakikisha haki za kibinadamu za wakimbizi wa ndani zinaheshimiwa ikiwemo kuwapatia makazi mbadala yaliyosa salama.

UNHCR inasema robo tatu ya watu hao ni wanawake na watoto na wanalala kwenye mashamba ya migomba.

Nchini DRC kwa sasa kuna wakimbizi wa ndani wapatao Milioni Moja na Nusu wakiwemo 610,000 katika jimbo la Kivu Kaskazini pekee.