Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CTBTO yakutana Vienna kufuatia jaribio la nyuklia DPRK

CTBTO yakutana Vienna kufuatia jaribio la nyuklia DPRK

Kamati ya kuchukua hatua ya nchi wanachama wa Shirika la Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Silaha za Nyuklia, CTBTO, imekutana leo mjini Vienna, siku moja baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK kufanya jaribio la silaha za nyuklia, ambalo ilidai kuwa jaribio la bomu la haidrojeni. Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Kamati hiyo inakutana ili kufanya tathmini ya mitetemeko iliyobainika jana kwenye eneo la DPRK la kufanyia majaribio ya nyuklia.

Taarifa kuhusu tathmini hiyo itatolewa kwa vyombo vya habari muda mfupi baada ya mkutano huo wa leo.

Tayari, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amelaani jaribio hilo la nyuklia lililofanywa na DPRK, huku Baraza la Usalama pia likililaani na kulitaja kama ukiukwaji wa maazimio yake kuhusu majaribio ya silaha za nyuklia.

Akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya simu kutoka Ouagadougou, Katibu Mtendaji wa CTBTO Lassina Zerbo, amesema.

(Sauti ya Bwana Zerbo)

“Kweli ni ukiukwaji wa azimio ya Baraza la Usalama, ambalo lilipitishwa kwa kauli moja, likiitaka Korea Kaskazini kuheshimu upigaji marufuku majaribio ya nyuklia, na kujiepusha na kufanya majaribio kama hayo. Kwa kufanya jaribio hili, Korea Kaskazini inapaswa iwajibishwe.”

DPRK au Korea Kaskazini ni moja ya nchi chache ambazo bado hazijatia saini mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia, CTBT, ambao umepiga marufuku milipuko yote ya nyuklia.