Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wayakumbuka mauaji ya kimbari Rwanda

Umoja wa Mataifa wayakumbuka mauaji ya kimbari Rwanda

Rais wa Baraza Kuu, Vuk Jeremic, amesema katika miaka baada ya mauaji ya kimbari, Wahutu na Watutsi nchini Rwanda wameweza kuja pamoja na ari mpya, ili kujenga nyumba ya haki na maendeleo kwenye msingi wa umoja na maridhiano, chini ya uongozi wa rais Paul Kagame.

Katika kipindi cha takriban siku mia moja, yapata watu laki nane waliuawa nchini Rwanda katika matukio ambayo Bwana Jeremic amesema yaliushangaza ubinadamu kwa kiasi kikubwa.

Amesema licha ya matukio hayo, watu wa Rwanda bado wamejitolea kuhakikisha kuwa ulipizaji kisasi unaepukika.

“Ukarabati wa Rwanda umekuwa mgumu na umechukuwa muda mrefu, lakini matokeo ya kujikwamua tena yanaonekana, kwa sababu ya nguvu na uvumilivu wa taifa lenye sifa, ambalo sasa lina uongozi wa kisheria, na wale wenye kusababisha maafa kuwajibika kisheria.

Kama rais wa Baraza Kuu, napongeza ufanisi wa Rwanda wa hivi karibuni, unaodhihirishwa kwa jamii kuishi pamoja, kwa hamu ya kuokoa vizazi vijavyo kutokana na vita.”

Akiongea kuhusu kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema Rwanda imepiga hatua kuendeleza jamii yenye amani na haki, na kuwasihi watu na serikali ya Rwanda kuendelea kuendeleza moyo wa ujumuishaji wa wote, ambao ni muhimu kwa ajili ya kuponya na maridhiano.

“Umoja wa Mataifa umeahidi kuiga kutoka kwa Rwanda na kusaidia jamii ya kimataifa kuzuia majanga siku zijazo. Kamwe tusiwasahau wahanga na kuhakikisha kuwa wanapokea msaada wanaouhitaji. Ni kwa kukabiliana na changamoto tulizo nazo tu ndipo tunaweza kuwaenzi waliokufa kwa ukatili usio na maana katika mauaji ya kimbari Rwanda miaka 19 iliyopita.”

Bwana Ban amesema mshauri wake maalum kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari hufuatilia hali kutambua ishara za uhalifu huo kabla utendeke. Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unaimarisha uwezo wake wa kushiriki mashauriano ya amani, kutafuta ukweli na kusuluhisha mizozo kwa njia ya amani.