Kushikiliwa kwa meli ya kivita Libertad, pande zote ziheshimu sheria za kimataifa: Jeremić

22 Oktoba 2012

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Vuk Jeremić leo amekuwa na mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Argentina, Hector Timerman ambapo Waziri huyo amemtaarifu juu ya kushikiliwa kwa meli ya kivita ya nchi hiyo, Libertad kwenye bandari ya Tema nchini Ghana.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani Bwana Timerman ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya kushikiliwa kwa meli hiyo.

Bwana Timerman ameitaka Ghana iheshimu mkataba wa umoja wa Mataifa juu ya sheria ya bahari pamoja na mkataba wa kimataifa wa mwaka 1962 unaojumuisha baadhi ya kanuni kuhusu kinga dhidi ya vyombo vya majini vinavyomiliwa na serikali.

Kwa upande wake Bwana Jeremić amesisitiza umuhimu wa nchi zote wanachama kuzingatia wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kueleza kuwa yuko tayari kusaidia pande zote kupatia suluhu suala hilo.